AOMBA WABUNGE KUCHANGIA POSHO ZAO KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Profesa Mark Mwandosya ameomba Bunge Maalumu la Katiba, kukata posho ya siku moja ya wajumbe wote wa Bunge hilo ili kuwapa pole waathirika wa mafuriko nchini, ikiwa ni pamoja na viongozi waliopata ajali ya helikopta.
Profesa Mwandosya alitoa pendekezo hilo kwa Bunge,  baada ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kutoa taarifa ya maendeleo ya afya za viongozi waliopata ajali ya helikopta jijini Dar es Salaam wakati wakitathimini maafa ya mafuriko hayo. Alisema wanaendelea vizuri.
Baada ya taarifa hiyo, Profesa Mwandosya aliomba mwongozo wa Mwenyekiti na kutoa pendekezo hilo la kutaka Bunge kukata posho ya siku moja ya wajumbe wote kutoa pole kwa waathirika wa mafuriko hayo.
Akijibu mwongozo huo, Sitta alisema kwa vile suala hilo lilikuwa halijajadiliwa na Kamati ya Uongozi ya Bunge, isingekuwa rahisi kwake kukubaliana au kukataa pendekezo hilo na hivyo alisema ataliwasilisha kwenye Kamati hiyo  kupata uamuzi.
Katika hatua nyingine, Sitta amesema mjumbe yeyote wa Bunge hilo ambaye ataona hatendi haki katika uendeshaji wa Bunge hilo kuwasilisha malalamiko yake kwa Kamati  ya Kanuni na Haki za Bunge.
Aliyasema hayo bungeni mjini hapa jana wakati akijibu mwongozo wa Mjumbe wa Bunge hilo, Dk Hamisi Kigwangala aliyemtuhumu Sitta kuwa anafanya upendeleo katika uendeshaji wa bunge hilo kwa kuwapendelea wajumbe walio wachache.
Kigwangala alisema kwa vile Sitta alimpa nafasi maalumu  Msemaji wa walio wachache wa Kamati Namba Nne, Tundu Lissu kutoa ufafanuzi baada ya kukatika matangazo ya TBC 1 Jumamosi, yeye pia anastahili kupewa nafasi hiyo kwa vile matangazo yalikatika  akiwasilisha maoni ya Kamati hiyo.
Akijibu mwongozo huo, Sitta alisema alimwagiza Katibu wa Bunge kufuatilia. "Baadaye Katibu wa Bunge alinitaarifu kuwa baada ya kuwasiliana na watu wa TBC 1  na walipofuatilia namna matangazo hayo yalivyokuwa yakirushwa hawajabaini kama kuna mahali yalikatika wakati Dk Kigwangala akizungumza, hivyo hoja yake ikakosa nguvu," alisema Sitta.

No comments: