'MUUNGANO HAUKUWA UAMUZI WA NYERERE NA KARUME'

Bunge Maalumu la Katiba limeelezwa kuwa si kweli kwamba muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania, haukuwa na ridhaa ya wananchi kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.
Badala yake, Bunge hilo limeelezwa kwamba ukweli ni kwamba viongozi wa kitaifa wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amaan Karume, walipata ridhaa ya wananchi kwa utaratibu uliofaa kwa wakati ule, kabla ya kufikia maridhiano wao wawili.
Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Kamati Namba Nne ya Bunge hilo, Dk Khamis Kigwangala alipokuwa anasoma maoni ya Kamati hiyo baada ya kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba mpya kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Christopher ole Sendeka.
Kigwangala alisema kwa vigezo na vipimo vya leo, utaratibu uliotumika wakati ule ambapo idadi ya watu ilikuwa ni ndogo ukilinganisha na leo, idadi na viwango vya uelewa vilikuwa vidogo ukilinganisha na leo, mifumo ya mawasiliano na viwango vya kiteknolojia, ikiwemo masuala ya mawasiliano ya habari vilikuwa ni vidogo, umuhimu wa uamuzi wa kidemokrasia ni muhimu zaidi leo kuliko hata mwaka 1964.
Alisema kero za Muungano katika muundo wa serikali mbili uliopo, nyingi zimetatuliwa, lakini nyingine kadhaa kubwa na ndogo zimeorodhosheswa katika Ibara ya 269 ya Rasimu ya Katiba mpya na ambayo imeweka wazi utaratibu mahsusi wa kuzishughulikia na kuzitatua kwa kuweka Tume Maalum chini ya Ibara ya 109 ya Rasimu.
“Uwepo wa mapendekezo ya kuunda Tume ya Uhusiano na uwepo wa maandalizi ya kutatua kero za Muungano, chini ya Ibara ya 110 (d) ya rasimu ya Katiba mpya unadhihirisha kuwa hata Muundo wa Serikali Tatu unaopendekezwa na Tume kwenye Katiba mpya si muarobaini wa kero za Muungano, “ alisema Kigwangala.
Alisema mtazamo wa wajumbe walio wengi wa kamati hiyo ilikuwa kwamba  mfumo wa utawala wa nchi ni msingi muhimu katika uandishi wa Katiba ya nchi yoyote ile duniani na kwa vile mfumo wa utawala wa Tanzania ni wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa nchi moja, Serikali  mbili, uwepo wa Muungano katika mfumo huo ni lazima uheshimiwe.
“Mheshimiwa Mwenyekiti katika nchi inayoheshimu na kusimamia misingi ya kidemokrasia kama hii ya kwetu, jambo la muundo wa Muungano ni jambo linaloingia moja kwa moja miongoni mwa mambo yanayopaswa kupata uhalali wake kutoka kwa wananchi kupitia mijadala mipana ya kitaifa na kura ya maoni na si kujadiliwa na kufanyiwa uamuzi na watu wachache kwa kutumia busara na hekima zao.”
Aidha Kigwangala alisema misingi mikuu ya kidemokrasia haitoa fursa hata kidogo kwa chombo cha kisheria kama Tume ya Mabadiliko ya Katiba kujipa mamlaka yasiyokuwepo kisheria, mfano mamlaka makubwa ya kubadili muundo wa Muungano ambayo ilijinyakulia kutoka mikononi mwa wananchi kinyume cha sheria ya mabadiliko ya Katiba, sura ya 83.
“Mheshimiwa Mwenyekiti kufanya hivyo ni kuondoa uhalali wa uamuzi huo na ni kwenda kinyume na misingi ya kidemokrasia ambayo siku zote Taifa letu limekuwa likiilinda, kuiheshimu na kuisimamia,” alisema.
Alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83, kifungu cha 9 (2) kinatoa maelezo kwa Tume juu ya mambo ambayo yalipaswa kuhifadhiwa na kudumishwa, miongoni mwake ni pamoja na kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano, uwepo wa Serikali, Bunge na Mahakama, mfumo wa kiutawala wa kijamhuri, uwepo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Umoja wa kitaifa, amani na utulivu.
Alisema mapendekezo ya Tume kwenye rasimu yanabadilisha muundo wa Muungano na hayakuzingatia sheria na kanuni mbalimbali za kidemokrasia katika kufanya hivyo.
Kuhusu maoni kinzani kwa Kamati hiyo, Kigwangala alisema wajumbe walio wachache walionesha jinsi ambavyo kero za Muungano katika muundo wa Serikali Mbili zimekuwa sehemu ya historia yote ya Muungano.
Alisema wachache hao walisema kwa mujibu wa Katiba ya Muungano, kero hizo zinazohusu tafsiri ya masuala ya Muungano zilitakiwa kuamuliwa na Mahakama maalum ya Katiba iliyoundwa chini ya Ibara ya 125 ya Katiba.
Katika hatua nyingine, akiwasilisha maoni ya Kamati Namba Tatu, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Francis Michael alisema kwa maoni ya wajumbe walio wengi Ibara ya Kwanza ya Sura ya Kwanza ya Rasimu ya Katiba inakiuka sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, toleo la 2014 kifungu cha 9 (2) (a), kinachoeleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iendelee kuwepo.
Dk Michael alisema pendekezo la kuwa na Shirikisho ni kwenda kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Ibara ya 9 (2) (a) ya sheria hiyo, pili kutasababisha ama kudhoofisha au kuuvunja kabisa Muungano, na hivyo kuibua dhana ya utaifa, kwenye nchi hizo mbili kitu ambacho ni hatari kwa Muungano uliopo.
“Kuvunjika huku kwa Muungano kunakozungumzwa na wajumbe walio wengi kwenye Kamati, kumezingatia uzoefu wa nchi zilizowahi kuwa na Muungano wa Shirikisho kama inavyopendekezwa kwenye rasimu ya Katiba inayopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kwa maoni ya wajumbe walio wengi wa Kamati hii, Ibara ya Kwanza ya Sura ya Kwanza kuweka kifungu kinachopendekeza Tanzania kuwa ni Shirikisho kimeondoa hata uhalali wa kuzijadili Ibara nyingine nyingi zinazoendelea katika rasimu hii kwa sababu Ibara nyingi zinazofuata kwenye rasimu hii iliyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba yameakisi muundo wa Shirikisho,” alisema Dk Michael.
Alisema uzoefu wa matatizo ya muundo wa kishirikisho unaotajwa na wajumbe walio wengi umehusisha Muungano wa nchi kama Misri na Syria, Senegal na Gambia ambazo ziliungana kishirikisho na muungano huo kutodumu, jambo ambalo ni hatari.
Akisoma maoni ya wachache, Mchungaji Peter Msigwa aliyepewa nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta baada ya wajumbe hao kupoteza imani ya maoni yao kusomwa na Dk Michael, alisema maoni ya wajumbe wachache kuhusu Ibara na Sura ya Kwanza yanasisitiza kwqamba madhumuni ya Ibara hiyo yabaki kama yalivyo kwa sababu ya msingi kuwa Muungano unatokana na makubaliano ya Muungano.
Mchungaji Msigwa alisema kutokana na makubaliano hayo ya Muungano tangu mwaka 1964 jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ulikua na sura ya Shirikisho na hivyo  alisema ni lazima Katiba mpya ikatambua jina hilo kama ilivyopendekezwa na Tume ya Katiba.

No comments: