MAFURIKO YASOMBA NYUMBA, MADARAJA NA KUUA WATATU DAR

Mvua iliyonyesha juzi na jana, ikiambatana na upepo mkali katika mikoa mbalimbali nchini, imeleta madhara na kusababisha vifo vya watu kadhaa.
Jijini Dar es Salaam, nyumba nyingi zimebomolewa na kuzingirwa na maji, na miundombinu imekatika, ikiwemo kufunikwa kwa madaraja muhimu na adha za kila aina.
Katika matukio ya vifo, watu watatu wamekufa, akiwemo mtoto Martin Mwambasha (3) aliyesombwa na maji katika eneo la Ubungo Msewe wakati akijaribu kuvuka.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 11:30 jioni. Mtoto huyo aliokolewa na kukimbizwa katika Zahanati ya Moyo Safi iliyopo Msewe. Lakini, daktari alibaini alikuwa ameshakufa na mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala.
Tukio la pili lilitokea eneo la Yombo Manispaa ya Temeke, ambako mtu mmoja, Mpuya Lufulisha (27), mfanyabiashara wa chipsi katika eneo la Yombo, alikufa baada ya kusombwa na maji.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo alisema mtu huyo alikufa wakati akijaribu kuokoa mkokoteni wake usichukuliwe na maji ndipo maji yalimzidi nguvu na kumzamisha kwenye mtaro na kufa. Mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke.
Tukio la tatu lilitokea huko Banana Ukonga, ambako mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Konga, anayekadiriwa kuwa na miaka 35-40 mkazi wa Majohe, alikufa baada ya kusombwa na maji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema mtu huyo alikuwa akitembea kwa miguu, ghafla alitumbukia katika shimo la maji na kunywa maji mengi na kisha kufa. Maiti yake imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mvua hizo zinazoendelea  kusababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali ya jiji hilo, huku yakiwaacha baadhi ya wakazi wa maeneo ya mabondeni wakiwa hawana pa kuishi.
Waandishi walitembelea katika maeneo hayo, ikiwemo Jangwani, Dar es Salaam, ambapo waliwakuta wakazi wa maeneo hayo wakihangaika kuokoa na kuhamisha baadhi ya vitu, ambavyo vilikuwa vikisombwa na maji.
Wakazi wa eneo hilo walipoona waandishi hao walianza kutoa maneno ya vitisho ili kuwaogopesha waandishi kufanya kazi yao, "Ukisikia ugaidi ndiyo huu, huku hatuhami ng'o, maana ndiyo kwetu na hatuwezi kuondoka. Na huko mnakoenda mtapigwa, kwani hamkuona sehemu nyingine ya kwenda kupiga picha zenu," alisikika dada mmoja ambaye jina lake halikufahamika.
Mmoja kati ya watu waliokuwa wakizunguka katika eneo hilo, kuangalia maji yaliyokuwa yakipita kwa kasi, alisema zilionekana maiti za watu zikielea katika maji.
"Kweli nisikudanganye mi mwenyewe nasikia tu kwamba kuna maiti zimeonekana hapa ila sijajua maana mi nimechelewa kufika hapa," alisema mtu huyo ambaye jina lake halikupatikana.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alisema daraja la mto Mpigi lilivunjika juzi na kusababisha adha kubwa kwa wasafiri.
Alisema zinazoendelea kunyesha, zimesababisha barabara nyingi katika wilaya hiyo, zisipitike kutokana na kufunikwa na maji.
"Pamoja na kuwa nyingi, mvua za kipindi hiki zimesababisha maeneo yasiyo na kawaida ya kufurika kama vile Mbezi Beach-Afrikana na Tegeta Basihaya yajae maji kiasi cha watu kuyakimbia. Hata hivyo, uongozi wa mkoa umekwishatoa mwongozo kuwa hatua za dharura zichukuliwe kuondoa maji hayo, ikiwa ni pamoja na kuzibua na kupanua mitaro iliyopo," Rugimbana alisema.
Alisema hadi jana wilaya yake ilikuwa na taarifa za vifo vya watu wawili waliosombwa na maji.
Alisema nyumba zote katika maeneo yenye mabonde, zimepitiwa na maji au kuzingirwa na mali kuharibiwa na maji.
"Eneo lote la Msasani linalopitiwa na bonde la Mpunga limejaa maji lakini uongozi wa wilaya unasimamia hatua mbalimbali za dharura zitekelezwe kuyaondoa. Tayari Tanroads wameanza kupanua mfereji mkubwa wa maji kwenye sehemu ya Mayfair hivyo tatizo litakwisha baada ya upanuzi kukamilika," alisema Rugimbana.
Ofisi za Kampuni ya MajiSafi na MajiTaka Dar es Salaam (DAWASCO) Tawi la Boko, nayo ilikuwa imezingirwa na maji.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Raymond Mushi alisema, athari kubwa imetokea  kwenye nyumba zilizojengwa mabondeni pamoja na madaraja yanayopitiwa na mito ya asili, likiwemo daraja linalounganisha wilaya za Ilala na Kinondoni, kupitia Tabata Kimanga.
Madaraja mengine yasiyopitika kwa sasa, kutokana na kingo zake kumomonyolewa na maji wilayani humo ni pamoja na linalounganisha barabara inayotoka eneo la Kilitex kuelekea eneo liitwalo Ulongoni B huko Gongo la Mboto. 
Mushi alitaja madaraja mengine yasiyopitika kwa sababu ya kuzidiwa na maji, kumomonyolewa kwa kingo na kufunikwa na maji kuwa ni pamoja na la Maji ya Chumvi, linaloiunganisha Tabata Kimanga na eneo linalojulikana kuwa ni la Jeshi na daraja linalotenganisha Tabata Kisiwani na Tabata Relini.
Kuhusu nyumba zilizofunikwa na maji, alisema ni za maeneo ya Tabata Relini kuelekea Kisiwani, Jangwani, Kipawa na kwingine kwenye mabonde.
Wakati huohuo, mwanaume mmoja ambaye hakufahamika alionekana akiwa juu paa la nyumba yake huku akiwa anawasiliana na simu kwa ajili ya kupata msaada wa kujinasua eneo hilo.
Wakazi wa eneo hilo, kwa upande wa Barabara ya Morogoro, walionekana wakiwa wamejihifadhi katika vituo vya mabasi yaendayo kasi wakiwa na mizigo yao.
Mafuriko hayo, pia yamekumba ofisi za Mradi wa Mabasi yaendayo Kasi (DART), ambapo pia wafanyakazi wake ambao ni raia wa China, walionekana wakikimbia huku wakiwa wamebeba mizigo yao.
Aidha, katika eneo la Ubungo External Darajani, nyumba takribani nne zimesombwa na maji, kutokana kuwa karibu na mto na hivyo kuwalazimu wakazi wa nyumba hizo kuondoka na kuelekea kusikojulikana.
Maeneo mengine yaliyokumbwa na mafuriko ni Kigogo, bonde la Mkwajuni, Bonde la Mpunga, Msasani, Mto Kizinga,  Mtoni Msikitini, Mazizini Ukonga na Mongo la Ndege Ulongoni.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), mvua hizo zitanyesha kwa siku nne mfululizo.
Mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Morogoro, zimeibua taharuki kubwa. Katika  Manispaa ya Morogoro katika Kata ya Mafisa,  nyumba zipatazo  200 zimezingirwa na maji.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mizambarauni katika kata ya hiyo, Hans Chamtwa alisema nyumba nyingine zipatazo 100, zimeingiliwa na maji na nyingine kubomoka.
Wakazi wa maeneo hayo, walikuwa katika wakati mgumu jana kutokana na  baada mvua hiyo kubwa ya siku. Kata zingine zilizoathiriwa ni  Mafisa, Kichangani, Mji Mpya na Kihonda.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, alipoulizwa kuhusu athari za mvua zinazoendelea,  alisema kwa wilaya ya Ulanga,   eneo moja ya Ilagua limeathirika, ambapo  barabara ya kutoka Ilagua kwenda Malinyi, imeharibiwa na mvua hizo na kusababisha zaidi ya magari 20 kukwama kwa siku ja
jana.
Kwa Manispaa, Mkuu wa Mkoa alisema  amearifiwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Jarvis Simbeye kuwa baadhi ya maeneo ya mitaa na Kata za Manispaa, zimekumbwa na mafuriko, lakini hakuna madhara makubwa ya kibinadamu.
Kwa upande wa wilaya ya Kilosa,  alisema hajapata taarifa kuhusu kutokea kwa mafuriko mapya, ikiwemo Tarafa ya Magole iliyoathirika hivi karibuni.

No comments: