MVUA YASABABISHA NDEGE YA KENYA AIRWAYS KUACHA NJIA DAR

Athari za mvua kubwa zinazoendelea kunyesha Dar es Salaam, jana zilifika mbali zaidi kwa kuikumba pia ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways).
Zaidi ya abiria 55 wa ndege hiyo walinusurika kufa baada ya ndege hiyo yenye namba KQ-482 kushindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam, kutokana na mvua na upepo mkali, uliosababisha ndege hiyo kuacha njia.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 8:15 mchana  baada ya ndege  hiyo, aina ya Embraer E190 kusukumwa hadi kwenye majani na  baadaye rubani aliirudisha  katika njia ya ndege. Baada ya hapo, ilitua salama katika uwanja huo.
Katika tukio hilo, abiria sita walijeruhiwa, wawili kati yao wakiwa katika hali mbaya na kulazwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Mkaguzi Mkuu wa ajali za ndege kutoka Wizara ya Uchukuzi, John Nyamwihula alisema baada ya kuirudisha kwenye njia hiyo, kuna kibati kiliingia katika injini ya kulia na kuibomoa, hivyo kuwalazimu abiria kushukia maeneo hayo.
Alisema katika kuhangaika wakati wa tafrani hiyo, watu sita walijeruhiwa, wakiwemo wawili walio katika hali mbaya, mmoja alivunjika mguu na mwingine mguu wake uliteguka na wamelazwa katika Hospitali ya Aga Khan.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Fadhili Manongi alisema baada ya kutokea kwa tatizo hilo, ndege hiyo ilivutwa na kuendelea na shughuli, isipokuwa ndege ndogo zilitua kwenye uwanja mdogo uwanjani hapo.
Alisema kutokana na tahadhari ya hali ya hewa, kuwa mvua itaendelea kwa siku tatu mfululizo, watafuatilia kwa karibu zaidi hali ya hewa na ikiwa itakuwa ya hatari,  watachukua hatua stahili.
“Kwa sasa tunaendelea kufuatilia, lakini hali ni shwari lakini ikiwa tutaona hali imezidi kuwa mbaya, itatulazimu kufunga uwanja, lakini kwa sasa hali siyo mbaya na shughuli zinaendelea kama kawaida,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Agness Kijazi alisema mvua zinazoendelea kunyesha ni kubwa mara mbili na zile za kawaida, kutokana na kufikia milimita 131  hadi milimita 135 kwa vituo viwili vilivyopimwa wingi wa mvua.
Alisema katika kituo cha Uwanja wa Ndege ilikuwa milimita 131 na bandarini milimita 135 kwa siku nzima ya juzi na jana jioni, wakati kwa kawaida mvua haziwezi kuzidi milimita 50 kwa siku.
Aliomba taasisi na wananchi kuendelea kuchukua tahadhari, kutokana na kuwa mifumo ya hali ya hewa inaonesha hali za mvua kuendelea hadi siku ya Jumatatu, kama ilivyokuwa imetabiriwa awali.
Dk Kijazi alisema bila kuchukua tahadhari, inaweza kuwa mbaya zaidi, kwani kama ilivyoonekana kwa siku moja tu mambo yamekuwa mabaya.

No comments: