MKAPA AHIMIZA WAFUGAJI KUPELEKA WATOTO SHULENI

Rais mstaafu Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ametaka jamii ya wafugaji wa Kimasai wilayani Monduli mkoani Arusha kuhakikisha inapeleka watoto wao.
Ameshauri wahakikishe wanasimamia na kufuatilia kikamilifu mienendo ya watoto wao wawapo shule kwa kuwa hiyo ni kazi yao na siyo ya mwalimu.
Mkapa alisema hayo jana wakati alipofanya ziara katika shule ya msingi ya wafugaji ya bweni ya Manyara Ranch iliyopo kata ya Makuyuni Wilayani Monduli, mkoani Arusha.
Alisema jamii ya kifugaji inapaswa kuamua kwa kasi ya hali ya juu kwa kupeleka watoto shule na kuhakikisha inafuatilia kwa ukaribu matokeo ya darasani ya watoto wao waweze kuwa wakombozi wa vizazi vijavyo.
Mkapa, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini wa Shirika la Uhifadhi Afrika la Afrika Wildlife Foundation (AWF),  alisema idadi ya watoto wa kifugaji  waliopo katika shule hiyo bado haitoshi.
Mkurugenzi wa AWF, John Swalehe alisema kuwa shirika lake lina mkakati madhubuti wa kutaka kuiweka shule hiyo katika nyanja ya kimataifa kwa kuweka ukarabati wa miondombinu ya huduma za kijamii kwa kutumia dola za Marekani 600,000.

No comments: