CRDB YACHANGIA SHEREHE ZA MUUNGANO WASHINGTON DC

Benki ya CRDB imekabidhi Sh 800,000 kwa ubalozi wa Tanzania nchini MarekaniÊ kuchangia gharama za maandalizi ya maadhimisho ya kihistoria ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Akikabidhi mchango huo kwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Liberata Mulamula, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya CRDB, Martin Mmari alisema mchango huo umetolewa kutokana na ombi la ubalozi huo kutaka kuungwa mkono na wadau mbalimbali katika kufanikisha maandalizi ya sherehe hizo.
Hafla hiyo iliyofanyika jijini hapa mwishoni mwa wiki, ilishuhudiwa pia na Mkurugenzi Mtendaji wa CRD, Dk Charles Kimei na maofisa wake waandamizi pamoja maofisa waandamizi wa ubalozi wa Tanzania nchini Marekani.
Mapema Balozi Mulamula alieleza kuwa kutokana na historia ya kuwa ni muungano pekee unaodumu mpaka sasa barani Afrika na kwamba mwaka huu unatimiza miaka 50, ubalozi wake umeandaa sherehe kamambe itakayohusisha shughuli mbalimbali makao makuu ya ubalozi huo jijini hapa.
Aliainisha shughuli hizo ni pamoja na sherehe ya kiserikali siku ya kilele cha maadhimisho hayo Aprili 26, itakayohusisha watanzania wanaoishi Marekani.
Itahusisha pia viongozi wa Marekani na mabalozi wa nchi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao. Kutakuwa na ngoma, maonyesho ya mavazi naÊ aina 25 ya mapishi ya vyakula vya kitanzania.
Kwa mujibu wa Balozi Mulamula, kutakuwapo na mkesha wa Usiku wa Mtanzania utakaohusisha dansi na shamrashamra nyingine.
Siku itakayofuata kutakuwepo mechi ya mpira wa miguu kati ya watanzania wanaoishi Marekani kutoka Zanzibar ikiwa na timu ijulikanayo kwa jina la Zanzibar Heroes na Bara timu iitwayo, Kilimanjaro Stars huku Balozi atakuwa wa kwanza kuanzisha rasmi pambano hilo.

No comments: