WALALAMIKIA BARABARA YA SINZA - MAGOMENI MOROCCO

Watumiaji  wa Barabara ya Sinza  hadi Magomeni Morocco kupitia eneo la kwa Mtogole, wameilalamikia  Manispaa ya Kinondoni  kwa kuchelewesha upanuzi wa barabara hiyo na hivyo kuhatarisha usalama wao.
Wakizungumza  kwa nyakati tofauti wananchi hao wakiwemo madereva wa daladala, walisema ufinyu wa barabara hiyo unaochangiwa na kona za 'hapa na pale' unahatarisha usalama wao.
Mkazi wa Tandale kwa Mtogole, Mussa Abdalla (72) alisema ufinyu wa barabara hiyo katika eneo hilo unaochangiwa na uwepo wa kituo kisicho rasmi cha daladala, unawasababishia msongamano wa magari.
Jamson Bulaya, dereva wa daladala linalofanya safari kati ya Ubungo na Msasani, alisema mbali na ufinyu wa barabara hiyo kuwapo kwa mashimo kunaleta kero kwa watumiaji mbalimbali.
Aliitaka Manispaa kuchukua hatua za haraka kuondoa tatizo hilo kwa kuwa linasababisha foleni zisizo za lazima na hivyo kupunguza ufanisi wa shughuli zao.
Ofisa Habari wa Manispaa hiyo, Sebastian Mhowera alisema upanuzi wa barabara hiyo upo katika mpango wa haraka wa manispaa hiyo na tayari wananchi wanaopaswa kusogezwa kupisha upanuzi huo wameshalipwa fidia.
Alisema kwa sasa wapo katika mchakato wa kumpata mkandarasi wa ujenzi wa barabara hiyo inayotarajiwa kuhusisha vituo vya daladala pamoja na mitaro inayowezesha maji kupita kwa urahisi.

No comments: