MADIWANI WA ZANZIBAR WATOA POLE KWA JIJI LA DAR

Madiwani wa Manispaa ya Zanzibar, wametoa pole kwa uongozi wa Jiji la Dar es Salaam  kutokana na mafuriko yaliyoikumba hivi karibuni na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 25.
Akizungumza jijini Dar es Salaam juzi siku ya kwanza ya ziara yao ya siku nne,  Meya wa Manispaa ya Zanzibar, Khatibu Abdurahaman Khatibu,  alisema kilichotokea ni mipango ya Mungu na hata wao limewagusa.
Alisema suala la mafuriko, halijapangwa na mtu na ni muhimu kila mmoja ashiriki kuwaombea na kuwasaidia wale waliofikwa na maafa  hayo, yaliyosababishwa na mvua iliyonyesha kwa zaidi ya siku tatu maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo jijini Dar es Salaam.
"Ndugu zetu  naomba mtambue kuwa tatizo hili nasi limetugusa  sana, kikubwa tuzidi kushirikiana kwa pamoja bila kutengana na Mwenyezi Mungu atatusaidia," alisema Khatibu.
Akizungumzia  malengo ya ziara yao, Khatib alisema lengo lake ni kudumisha ushirikiano baina  yake na Manispaa ya Kinondoni.
Alisema anaamini ushirikiano huo, utasaidia katika kuziletea maendeleo manispaa hizo, hivyo kuwapa wananchi unafuu wa maisha.
Aidha, alisema mbali na masuala mengine, ziara hiyo imelenga kudumisha Muungano wa Tanzania, unaotarajiwa kuadhimishwa Aprili 26.
Aliwataka wananchi wa pande zote mbili, kuulinda kama ilivyokusudiwa na waasisi wa Muungano huo.
Mmoja wa madiwani hao wa Zanzibar, Sharah Ahmed alitoa pole kutokana na  mafuriko hayo na pia aliwataka wajumbe wenzake kujifunza mambo mazuri yanayohusu maendeleo ya Manispaa ya Kinondoni  ili baadaye wayachukue kwa ajili ya faida ya Manispaa yao ya Zanzibar.
Kwa upande wake, mwenyeji wao, Meya wa Manispaa ya Kinondoni,  Yusufu Mwenda alisema zaidi ya Sh bilioni 12 na milioni 600 zinahitajika ili  kurejesha hali ya miundombinu iliyoharibika na mvua katika manispaa hiyo.
Alisema  madhara yaliyosababishwa na mvua hiyo ni makubwa huku akiwataka wananchi kuheshimu kauli  za Serikali, zinazowataka kuondoka  katika maeneo ya mabondeni ili waepukane na maafa  ya mara kwa mara.

No comments: