PENGO AHIMIZA WATANZANIA KULIOMBEA BUNGE LA KATIBA

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycap Kardinali  Pengo, ametuma salamu za Pasaka kwa Watanzania wote huku akisisitiza kuliombea Bunge Maalumu la Katiba.
Alisema hayo jana Ofisini kwake Dar es Salaam na kufafanua kuwa Pasaka ya mwaka huu, imefika wakati mwafaka kwa kuwa  Bunge Maalumu la Katiba lipo katika mchakato wa kupata Katiba mpya, hivyo waumini wasali kuombea Bunge hilo.
Alisema kwa pamoja Watanzania wanapaswa waombee Taifa   ili Katiba ifanikiwe na iwe yenye matunda ya kudumu kwa wote.
Aliwataka Wakristo waombe kupitia Mwinyiheri Baba Mtakatifu Paul wa Pili, ili Katiba hiyo idumishe amani, upendo   Taifa liwe moja kama Serikali ya Tanzania na Zanzibar.
Alisema maombi hayo yatamfurahisha Papa Paul wa Pili huko aliko kama bado tutauendeleza Muungano wa nchi hizi.
Padre wa Kanisa la Bikira Maria, Mama wa Mwokozi Sinza, Cuthbert Maganga aliwataka Wakristo wote kuishi upendo unaovuka mipaka na sio kubagua na kujitafutia faida kupitia wengine.
Alisema wanatakiwa kuwajali wenye shida mbalimbali ili Pasaka hii, iwe ya kipekee na yenye matunda bora kwa waumini na Watanzania wote.

No comments: