KAULI YA MAGUFULI YAWASIKITISHA WAKAZI WA KIVULE

Wananchi katika eneo la Kivule, katika Wilaya ya Ilala wamesikitishwa na kauli ya Waziri wa Ujenzi, Dk John  Magufuli kwamba madaraja yote katika Jiji la Dar es Salaam, sasa yanapitika, wakati eneo la Kivule bado halipitiki, baada ya kuharibiwa na mvua wiki iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Daraja la Mto Mzinga,  mmoja wa wakazi wa eneo hilo, James Temba alisema taarifa ya Magufuli imewafanya wajisikie  wao si sehemu ya waathirika  wa mafuriko, yaliyolikumba Jiji la Dar es Salaam.
“Inasikitisha kwamba sisi tuko kilometa 22 tu kutoka Ikulu lakini Waziri mwenye dhamana ya Miundombinu ameshindwa kujua kuwa daraja letu limeharibika na kwamba hakuna ukarabati wowote uliofanyika,” alisema Temba.
Alisema baada ya kuona daraja hilo limekatika, waliamua kujitolea na kujenga daraja la muda na hakuna kiongozi yeyote katika ngazi ya Wilaya akiwemo, Meya, Mbunge wala Diwani aliyetoa ushirikiano katika ukarabati wa daraja hilo.
Temba alieleza masikitiko ya wananchi wa Kivule kwamba wakati wananchi, wakiongozwa na Klabu ya New Kivule Veteran,   wanashirikiana kujenga daraja hilo, chini ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, J.B. Gasaya,  kumekuwa na taarifa kwenye vyombo vya habari kwamba fedha zimechangwa kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo.
Daraja la Mto Mzinga linatumika na wananchi kutoka kata za Kitunda, Bombambili, Msongola, Chamazi, Mbondole, Magore na Mvuti.
Hali hiyo imefanya nauli ya daladala kupanda kutoka upande mmoja wa daraja kwenda Banana na Kitunda  kutoka Sh 400 za awali kwenda Sh 1,000.
Aidha, bei ya kukodi pikipiki kutoka Kitunda hadi kwenye daraja hilo, imepanda kutoka Sh 1,500 hadi 3,500 na bei ya vyakula kama mchele, nyanya, vitunguu, mkaa na unga wa mahindi vimepanda kwa zaidi ya mara mbili.

No comments: