MADABIDA KUSOMEWA MAELEZO YA AWALI MEI 14

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Mei 14 mwaka huu kumsomea maelezo  ya awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Limited, Ramadhani Madabida na wenzake wanaokabiliwa na mashitaka ya kusambaza dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVs).
Hakimu Mkazi Nyigulila Mwaseba alisema hayo jana baada ya kuahirisha kesi hiyo kwa kuwa Wakili wa Serikali Shedrack Kimaro hakuwepo mahakamani.
Mbali na kushitakiwa kwa kusambaza dawa hizo, Madabida ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, na wenzake wanadaiwa kusababisha hasara ya Sh milioni 148 baada ya kusambaza dawa hizo kupitia kiwanda chake cha TPL kwa Bohari ya Dawa Tanzania (MSD).
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni wafanyakazi wa kiwanda hicho, Mkurugenzi Uendeshaji Seif Shamte, Meneja Masoko Simon Msoffe na Mhasibu Msaidizi Fatma Shango, pamoja na wafanyakazi wa MSD ambao ni Meneja Udhibiti Ubora Sadick Materu na Ofisa Udhibiti Ubora  Evans Mwemezi.
Inadaiwa Aprili 5, mwaka 2011, Madabida, Shamte, Msoffe na Fatma waliisambazia MSD makopo 12,252 ya dawa bandia za Antiretroviral, ikionesha zimetengenezwa Machi 2011 na mwisho wa matumizi Februari mwaka jana pia walijipatia Sh milioni 148.35 kwa madai ni malipo halali ya dawa hizo.
Materu na Mwemezi wanadaiwa, kati ya Aprili 5 na 13, 2011, Dar es Salaam, wakiwa waajiriwa wa MSD, kwa nia ya kutenda kosa la kusambaza dawa hizo, walishindwa kutumia uwezo wao wote kuzuia kutendeka kwa kosa hilo.
Katika mashitaka mengine, washitakiwa wote wanadaiwa kati ya Aprili 5 na 30, mwaka 2011, kwa nia ovu au sababu za kutotekeleza majukumu yao vizuri, walisababishia MSD hasara ya kiasi hicho cha fedha, kutokana na kuwasambazia dawa bandia.

No comments: