WAJUMBE UKAWA WAREJEA KIMYAKIMYA BUNGENI KUDAI POSHO ZAO

Utamu wa posho katika Bunge Maalumu la Katiba, umeathiri siasa za baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo waliojiundia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wajumbe hao waliondoka bungeni kwa mbwembwe wakisusia vikao vya Bunge hilo na kudai hawarudi ng’o, lakini jana baadhi yao walirejea kinyemela bungeni na kwenda moja kwa moja Ofisi ya Katibu wa Bunge Maalumu, kudai posho za vikao ambavyo hawajashiriki.
Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta juzi mchana alitangaza bungeni kuwa, amepata taarifa kuwa wajumbe wa Ukawa wamerudi lakini si katika vikao bali wameonekana kwa Mhasibu kuchukua posho.
“Kuhusu hilo la Ukawa kurudi, taarifa zilizonifikia hivi punde zinaeleza kuwa wamerudi, lakini wameenda kwa Mhasibu kuchukua posho,” alisema Sitta na kusababisha wajumbe waliokuwepo ndani ya Bunge hilo kucheka.
Baada ya Sitta kueleza hivyo, alimkaribisha Mjumbe Adam Malima, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha, kutoa taarifa kuhusu hatua hiyo ya Ukawa kurudi kuchukua posho.
Malima alisema utaratibu wa fedha zinazolipwa na Serikali ni kwa wajumbe wanaokuja katika kazi za Bunge hilo na kuongeza kuwa, Serikali haipo tayari kuwalipa watu ujira ambao hawajaufanyia kazi.
“Tumezungumza na Katibu wa Bunge na kukubaliana kwamba, wote wasio na mahudhurio malipo yao yasitishwe kwanza, hawawezi kuchukua fedha wakati hawajafanya kazi, hili tunaiachia Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu,” alisema Malima.
Baada ya Malima kumaliza kutoa taarifa hiyo, Sitta alisisitiza kuwa, wajumbe hao hawawezi kuchukua fedha kwa kugoma kufanya kazi iliyowapeleka Dodoma.
Akizungumza na mwandishi jana, Katibu wa Bunge hilo, Yahaya Khamis Hamad, alikiri kuwa baadhi ya wajumbe wa Ukawa walirudi kuchukua posho lakini hakuwataja majina.
Alisema juzi walitangaza wajumbe wajaze fomu kwa ajili ya malipo yao na inavyoonekana, baadhi ya wajumbe wa Ukawa, kwa kujua wahasibu hawawafahamu vizuri kama wapo bungeni ama ni miongoni mwa walioondoka, walichukua fomu na kujaza kuchukua posho.
“Kabla ya malipo yoyote, utaratibu wetu ni lazima wajumbe wajaze fomu za malipo, jana (juzi) tulitangaza wajumbe wajaze fomu kwa ajili ya malipo, Ukawa nao waliingia na kuna fomu walijaza, nimechukua orodha ya mahudhurio ili kujua waliohudhuria.
“Nimeagiza asubuhi hii fomu zote niletewe, ambaye hakuwa ndani hata kama si Ukawa ataeleza alikuwa wapi, kama hakuwa ndani hatutamlipa mpaka Mwenyekiti (Sitta) aidhinishe kwamba mhusika alikuwa na dharura ya muhimu akiwa Dodoma ndio atalipwa posho ya kujikimu lakini si ya kikao,” alisema Katibu huyo.
Alisema mjumbe yeyote atakayelipwa posho ya kikao ya Sh 70,000 ni aliyehudhuria kikao na kujaza fomu lakini posho ya kujikimu ya Sh 230,000, italipwa kwa mjumbe aliyefika Dodoma kwa ajili ya Bunge hata kama alipata dharura ya kutohudhuria vikao kadhaa.
Kwa mujibu wa Yahaya, posho zinazolipwa ni za kuanzia Aprili 19 mwaka huu hadi Aprili 26 na kwamba za kuanzia Aprili 18 kurudi nyuma, zote zilishalipwa.
Hata hivyo, alifafanua kuwa posho ya kujikimu pamoja na kwamba hulipwa mjumbe akiwasili Dodoma, wapo wajumbe ambao hawajalipwa kutokana na kukosekana ufafanuzi wa dharura zao lakini maelezo ya Sitta ya uthibitisho yakitolewa, watalipwa.
Akizungumzia kuhusu uamuzi wa Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu  iliyokuwa ikae Alhamisi iliyopita kujadili hatma ya posho za wajumbe wa Ukawa, Yahaya alisema kikao hicho hakikufanyika.
Alifafanua kwamba sababu ya kutofanyika kikao hicho ni kutokuwa na taarifa kamili kwa kuwa Sitta aliomba kwenda Zanzibar, kukutana na baadhi ya viongozi wakiwemo wa Ukawa kutafuta suluhu.
Katibu alisema Kamati ya Uongozi inaweza kukutana muda wowote kuanzia sasa kwa kuwa Sitta amesharejea bungeni.
Sitta alikwenda Zanzibar Jumatatu wiki hii, ambapo   pamoja na kukutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Seif Sharif Hamad, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi-CUF, pia alikutana na Rais wa SMZ, Dk Ali Mohamed Shein na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

No comments: