Kutolewa hadharani kwa Hati ya Muungano, kumeanza kuwachanganya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waliojiundia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Hali hiyo imejitokeza wakati baadhi ya wajumbe wa Ukawa walipozungumza na gazeti hili kuhusu hatua ya Serikali kuweka hadharani hati hiyo juzi.
Akizungumzia hatua hiyo ya Serikali, Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe alijikuta akianza kumlinda mjumbe mwenzake maarufu, Tundu Lissu, kwamba alisema hati hiyo haipo kutokana na mazingira.
Alidai kuwa mazingira hayo yanatokana na baadhi ya Tume na viongozi wa Serikali kudai kuiona hati hiyo bila mafanikio, huku akidai bado watatafuta hoja ya kutaka kuhakiki uhalali wake
“Serikali imetangaza imeonesha kile kinachoitwa Hati ya Muungano, kumetokea kubeza kwingi hususan kwa wajumbe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakipotosha alichosema Tundu  Lissu bungeni kwamba Hati hiyo haipo na sasa imeonekana, hoja ya Lissu inatokana na ushahidi wa kimazingira, hati hii imetafutwa muda mrefu… leo ghafla imeonekana?” alihoji Freeman Mbowe.
Lakini wakati Mbowe akitoa hoja hiyo, Mjumbe Ismail Jussa Ladhu, aliishukuru Serikali kwa kuitoa hadharani hati hiyo na kusema Serikali imetambua umuhimu wa matakwa ya Ukawa.
Wajumbe hao wa Ukawa, walitumia muda mrefu katika Bunge hilo hilo kupotosha umma kuwa hati hizo hazipo, na walipopewa sheria ya kuridhia Muungano, nayo wakaipinga wakidai imechakachuliwa.
Msingi wa kudai haki hiyo huku wakipotosha kuwa haipo, ulikuwa kujenga hoja ya kubatilisha Muungano uliodumu kwa miaka 50 na kuipa nguvu hoja ya muundo wa serikali tatu.
Kutokana na upotoshwaji huo, Rais Jakaya Kikwete aliridhia hati hizo zioneshwe hadharani na nakala zilizothibitishwa kisheria zipelekwe bungeni kuondoa upotoshwaji huo na kuwekwa katika Makumbusho ya Taifa, kwa ajili ya wananchi kujionea.
Juzi Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, ilipokuwa akionesha hati hiyo,  alisema hati hiyo ipo, ilikuwepo siku zote na kufafanua kuwa ni lazima baadhi ya hati muhimu zihifadhiwe kama mboni ya jicho.
“Lazima tukubaliane kuwa zipo hati fulani ambazo ni kiini cha uwepo wetu kama Taifa huru, Jamhuri huru na Muungano huru, ambazo tunazihifadhi kama mboni ya jicho.
 “Hati hizo ni pamoja na Hati ya Uhuru wa Tanganyika ya mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962, na Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964.
“Hati za aina hii zinahifadhiwa maeneo maalumu ambayo ni salama ili zisipotee wala kuharibika. Kwa kawaida hatuzitoi, tunazihifadhi kwa namna yoyote ile,” alisema Balozi Sefue.
Wakizungumza jana na mwandishi katika Viwanja vya Bunge, mjini hapa kuhusu kupatikana na kutolewa kwa hati hiyo, baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo walisema kwa nyakati tofauti kuwa, mjadala kuhusu kuwepo ama kutokuwepo kwa Hati ya Muungano unapaswa kufungwa sasa.
“Kimsingi hati kuwepo ama kutokuwepo haikuwa hoja ya msingi, hata ikiwa zimepatikana, wapo watakaokuja na jipya, wapo watu wanataka kukwamisha Muungano, wanahoji hati leo wakati waliapa kutii Jamuhuri ya Muungano, Muungano upi wasioutambua walipoapa?
“Ni sawa na mtoto kuhoji ndoa ya baba na mama si halali ilifungwa na Mzungu ama Mwafrika, si sawa,” alisema Mjumbe wa Bunge hilo, Charles Mwijage.
Mjumbe mwingine, Ali Keissy alisema mjadala kuhusu hati haupaswi kuendelea kupoteza muda, unatakiwa kufungwa na kutoa fursa kwa wajumbe kuunda Katiba yenye tija na maslahi ya umma, huku akionya mwendelezo wa mipasho ndani ya Bunge hilo, ni ukuta mwingine unaozuia kupatikana kwa Katiba nzuri.
“Katika jambo la msingi kama hili, watu walidai hati, imefika, suala hili tulifunge, tusiibue mapya, ila kinachosikitisha zaidi ni mwenendo wa Bunge hili, ni mipasho na utoto mtupu ndani humo, kwa mwenendo huu, hakuna Katiba mpya yenye tija, watu wanachambuana mambo binafsi ya kuolewa, kuoa na kuwa na watoto, hatujatumwa hayo na Watanzania,” alisema Keissy.
Katika hatua nyingine, Mjumbe, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Waride Bakari Jabu, alisema Wazanzibari wanaunga mkono muungano wa serikali mbili na wanaopinga, wengi wao walikwenda Zanzibar kwa mbio za Mwenge.
Alimtaka Makamu wa Kwanza wa Zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad, kutowalaghai Watanzania kwamba Wazanzibari hawataki Muungano wakati wanachama wa CUF ndio wasioutaka.
Alisema wapo wachonganishi wa muungano na hao ndio wanaohoji uhalali wa Muungano wakitaka uvunjike.
 “Na sisi tunataka Hati ya Makubaliano kati ya Unguja na Pemba iletwe hapa tunataka kuiona, Wanzanzibari wa CUF ndio wanataka kuvunja Muungano, wanasema Wazanzibari wote hii si kweli,” alisema Jabu.
Naye Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Ezekia Maige, alipokuwa akizungumzia hoja ya gharama za serikali tatu, alitumia takwimu zilizowasilishwa na Mbowe kuelezea umuhimu wa serikali mbili.
Alimkariri Mbowe akielezea kushangazwa na hoja ya gharama katika muundo wa serikali tatu, wakati asilimia takribani 35 hadi 40 za fedha nchini zinatumika vibaya kwa mafisadi na masuala mengine yasiyo na tija kwa wananchi.
Maige yeye alisema kama mianya hiyo ya rushwa na ufisadi itakomeshwa, fedha hizo zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo na sio kugharimia muundo wa serikali tatu.
Alipokuwa akizungumzia faida za Muungano, alisema ni wazi  Zanzibar imenufaika, ingawa pamoja na manufaa hayo yote bado yapo malalamiko kwamba upande huo unanyonywa.
Alisema Muungano una faida kwa pande zote na suala la kusema Zanzibar imeonewa sio kweli kwani hata sasa  wilaya zote 10za Zanzibar zina barabara za lami na miundombinu yao ni mizuri kuliko wilaya za Bara.
Naye mjumbe Mwigulu Mchemba, alisema Tanzania Bara imekuwa ikikusanya Sh trilioni 7.7 kwa mwaka  na kati ya hizo Sh trilioni nne zimekuwa zikitumika kulipa mishahara.
Alifafanua kuwa Sh trilioni tatu zinazobakia, ndizo zimekuwa zikipelekwa kuwahudumia wananchi katika kutoa elimu, maji, mikopo ya elimu ya juu na kadhalika.Alihoji kwa kuwa rasimu ya Katiba inataka Sh trilioni tatu zitumike kuendesha serikali ya Shirikisho, fedha za maji, miundombinu, elimu na huduma zingine zitatoka wapi?
Alisema kama serikali tatu zitapita, ataongoza kundi la vijana wasio na ajira kupinga ongezeko la gharama katika utawala na uendeshaji, ili fedha zaidi zipelekwe katika kuhudumia wananchi waone thamani ya fedha ya kodi zao.
Naye Mjumbe  Panya Ali Abdallah, alielezea kuwashangaa wajumbe wa bunge hilo wanaotoka  Ukawa upande wa Zanzibar, wanaounga mkono hoja ya kuwa na serikali tatu.
Alisema wajumbe hao wa  Zanzibar  wamedandia hoja hiyo kwani wameikuta Dodoma na hoja waliyokuja nayo ilikuwa  serikali ya Mkataba.
“Hao wachache kutoka Zanzibar wasiseme Wazanzibari wotehawataki Muungano, waseme ukweli wao wanataka serikali ya mkataba tena wanaita ”nkataba” ndio hoja yao toka Zanzibar sasa wamefika hapa wamekuta hoja ya serikali tatu na wao wanaidandia,  si wakweli hao, waseme hiyo yao ya“Nkataba” mbona hawaisemi?” Alihoji Panya.
“Sisi tunaamini mapinduzi ya mwaka 1964 na ndio msimamo wetu hatutaki kurudishwa nyuma kwanza Zanzibar tuna wasiwasi wa kuja tena kwa Sultani, ila wapo wanaobeza na hatuwashangai kwa sababu hawataki Muunganowanatafuta  njia nyepesi ya kurudi kwa mkoloni”, alisema Panya.
Alisema awali Wazanzibari waliomba wawe na serikali ya Umoja  wa Kitaifa na leo wameipata, lakini cha ajabu hata serikali hiyo haijamaliza kipindi cha kwanza cha utawala wanaibuka watu na kutaka kuvunja Muungano huo.
“Tusivunje Muungano eti kwa kuwa kuna kero za Muungano, hata binadamu tuna kero na huenda zipo muda mrefu kuliko hata hizo za Muungano, tunaangalia jinsi ya kuzitatua na tuendelee na muundo wa serikali mbili na siotatu,” alisema Panya.
Akisisitiza hilo alimuomba Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad,  kukaa na wenzake na kukubaliana kuendelea kusimamia amani ya nchi na sio kuivunja kwani kufanya hivyo ni kuvuruga wananchi.
Akiunga mkono hoja hiyo, mjumbe kutoka Zanzibar WaridiBakari Jabu alisema Muungamo wa Zanzibar na Tanganyika una historia ndefu hivyo wanaoubeza ni wachache na wengi wao wanatoka Chama cha Wananchi (CUF).
“Wanaotaka kuvunja muungano ni CUF , na sio Wazanzibari wote, kwani ubaguzi umeanzia Pemba, na Seif Sharif  Hamad  ambaye aliiba nyaraka za Abdu Jumbe na kumpelekea Mwalimu Nyerere akidhani atapewa yeyemadaraka,” alisema Panya.
Kwa upande wake mjumbe kutoka Zanzibar, Mwinyi Haji Makame, alisema hoja ya serikali tatu kwa hao wachache wanaoitaka wameikuta Dodoma na kwamba muundo huo ni kutaka kuvunja Muungano.
“Huyo Sultani alitawala Zanzibar zaidi ya miaka 300,alivyoondoka aliwaachia nini Wazanzibari, hakuna lolote, lakini leo tunaona miaka 50 ya Muungano kuna manufaa mengi, tunaamini Mapinduzi ndio Muungano na havitenganishwi kamwe , asiyeweza arudi kwao,” alisema Makame.

No comments: