BARABARA ZILIZOATHIRIWA NA MVUA SASA ZAANZA KUPITIKA

Sehemu kubwa ya barabara zilizoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbali mbali  hususani jijini Dar es Salaam, zimeanza kupitika baada ya matengenezo ya dharura.
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo, alisema tangu jana  asubuhi tayari magari madogo  na mabasi yalianza kupitia katika eneo la Ruvu mkoani Pwani.
Alisema barabara ya Kilwa iliyokuwa imejifunga eneo la Mbagala Kongowe katika daraja la Kizinga imeweza kutengenezwa na watu pamoja na magari yalianza kupita tangu juzi usiku.
Alisema kwa upande wa daraja la Ruvu, tayari matengenezo yalikamilishwa jana asubuhi huku  katika barabara ya Kilwa, Dk Magufuli alishiriki katika usimamizi hadi usiku, hivyo magari na watu walianza kupita usiku huo huo katika barabara ya Kilwa.
Aidha alisema kwa sasa jitihada zimeelekezwa katika sehemu ya Mpiji kwenye barabara ya Dar es Salaam-Bagamoyo na eneo la Mtokozi katika barabara ya Kongowe - Mjimwema. Maeneo yote haya yanatarajiwa kuanza kupitika kuanzia leo jioni.

No comments: