MAJAMBAZI YAPORA FUKO LA FEDHA BENKI YA BARCLAYS

Majambazi wenye silaha wamepora fedha zinazokisiwa kufikia Sh milioni 300 katika Benki ya Barclays tawi la Kinondoni `TX  Market' jijini Dar es Salaam.
Mashuhuda wa tukio hilo, wamedai kuwa uporaji huo ulifanyika  saa nne za asubuhi, ambapo mtu mmoja aliingia eneo la benki hiyo akiwa na gari aina ya Cresta na kuwashusha watu wawili waliokuwa wamebeba begi linalodaiwa kuwa fedha na  kuingia ndani.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, mlinzi wa tawi hilo wa Kampuni ya Ulinzi ya Ultimate alifuata gari hilo na kuliekeza mahali sahihi pa kuegesha magari, kwani pale lilikuwa linazuia magari mengine kuingia benki.
Wakati mlinzi huyo akilielekeza gari hilo mahali sahihi pa kuliegesha, watu watatu walikuja na bodaboda wakiwa wamepakizana mshikaki, ambapo wawili walishuka wakaingia ndani huku mmoja akibaki nje na pikipiki hiyo ambayo haikuzimwa.
Inadaiwa watu hao wawili waliokuwa katika boda boda, wakiwa ndani ya benki hiyo, waliwaweka chini ya ulinzi wateja pamoja na wafanyakazi wote wa benki hiyo.
Baada ya muda, mashuhuda hao wamedai walimuona mlinzi aliyekuwa akielekeza gari mahali pa kuegesha, akipiga kelele na kukimbia huku na huko kuomba msaada.
Wakati mlinzi huyo akikimbia kuomba msaada, inadaiwa watu hao wawili waliokuwa ndani ya benki hiyo, walitoka na mfuko mkubwa unaodhaniwa kuwa na fedha na kupanda pikipiki waliyokuja nayo na kuondoka kwa kasi bila kukamatwa.
Hali hiyo ilisababisha watu kujitokeza kwa haraka kutoa msaada, huku taarifa zingine zikitolewa kwa askari Polisi ambao walifika muda mfupi baadae katika eneo la tukio na kufunga kamba eneo lote la benki na kuzuia watu kuingia katika eneo hilo wakati wakifanya uchunguzi wa awali.
Hata hivyo, haijajulikana kama walioingia awali na begi ndio waliokuwa na fedha zilizoporwa na wezi walitoka na begi, hivyo haijajulikana kama fedha hizo zilikuwa ni za wale wateja au la, kwa kuwa hakuna askari Polisi wala mfanyakazi yeyote wa benki hiyo aliyekuwa tayari kuzungumzia tukio hilo.
Taarifa zingine zilizopatikana eneo benki hiyo, zilieleza kuwa  nyuma ya tawi hilo kulikuwa na askari Polisi lakini sasa hawapo baada ya huduma hiyo kusisitishwa na benki hiyo ambayo iliamua kutumia walinzi wa kampuni binafsi, ambao hawakuwa na bunduki na badala yake walikuwa wanalinda kwa marungu.
Baadhi ya watu waliokuwepo eneo la tukio walilaumu taasisi za kifedha kwa kushindwa kuwatumia askari Polisi kwa ulinzi na badala yake wamekuwa wakizitumia kampuni za ulinzi, ambazo hazina silaha za uhakika."
Inashangaza sana taasisi za kifedha badala ya kuwatumia askari Polisi kwa ulinzi wa benki zao wenyewe, wameng'ang'ania kulinda kwa kutumia walinzi wa kampuni binafsi ambao hawana hata silaha, " alisema Juma Seleman ambaye ni mfanyabiashara katika eneo hilo.
Baadhi ya wananchi walilipongeza Polisi Kanda Maalum Kinondoni, kwa kuwahi kufika haraka eneo la tukio na kufika na vifaa tofauti na huko nyuma ambako walikuwa wakichelewa  kufika kila walipoitwa katika tukio.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alikiri kutokea kwa uporaji huo, ambapo alisema watuhumiwa hao walifika eneo hilo wakiwa na risasi za moto.
Hata hivyo, alisema kiasi cha fedha kilichoibwa bado hakijajulikana kwa kuwa watu wa benki hiyo walikuwa bado hawajamaliza kufanya tathmini lakini ni kiasi kikubwa."
Katika tukio hilo hakuna aliyejeruhiwa, kiasi cha fedha hakijajulikana lakini ni kiasi kikubwa cha fedha. Wakimaliza kufanya tathmini itajulikana ni kiasi gani," alisema Kamanda Wambura.

No comments: