KESI YA MRAMBA YADODA TENA MAHAKAMANI

Mawakili  wa upande wa utetezi jana wamekwamisha kuendelea kusikilizwa kwa kesi ya matumizi mabaya ya ofisi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake.
Hatua hiyo inatokana na mawakili hao kutofika mahakamani jambo lililosababisha Jaji Sam Rumanyika kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 23, mwaka huu itakapotajwa tena.
Juzi kesi hiyo ilitakiwa iendelee lakini iliahirishwa hadi jana kwa kuwa jopo la majaji halikukamilika pia pande zote mbili katika kesi hiyo hawakutimiza amri ya Mahakama iliyowataka kuwasilisha hoja za jinsi ushahidi wa aliyekuwa Kamishna wa Kodi, Felesian Msigala utakavyopokewa mahakamani ili kuunga mkono utetezi wa Mramba.
Mbali na Mramba, washitakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.
Wanadaiwa kuwa kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14, 2004 jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7.
Ilidaiwa kuwa walisababisha hasara hiyo baada ya kutoa msamaha wa kodi kinyume cha sheria kwa Kampuni ya M/S Alex Stewart ya nchini Uingereza.

No comments: