MWANAMKE KUJITAMBUA NA SARATANI KWA DAKIKA MOJA

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Shirika la Afya la PSI Tanzania wamegundua kifaa maalumu cha kugundua maambukizi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi ikiwa katika hatua ya awali ndani ya dakika moja.
Kutokana na kugundulika kwa kifaa hicho tayari wizara hiyo na PSI wameanza kufanya uchunguzi kwa wanawake wa Mikoa ya Tanga, Singida, Mbeya, Mwanza na Dar es Salaam ili kujaribu kuwaokoa wanawake watakaogundulika kuwa na ugonjwa huo katika hatua ya mapema.
Hayo yalisemwa  jana na Daktari Bingwa wa magonjwa ya wanawake, Dk Mashafi Joseph alipokuwa akizungumzia kufanyika kwa Jukwaa maalumu la kupima afya za wanawake maarufu kama Familia Kitchen Party Gala litakalofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Jumapili.
Dk Mashafi ambaye ni Mshauri wa Masuala ya Afya wa PSI alisema kupatikana kwa kifaa hicho kinachotoa majibu ya maambukizi ya saratani ya mlango wa kizazi katika muda mfupi kiasi hicho ni hatua zinazochukuliwa na serikali na PSI katika kupunguza vifo vya wanawake kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo afya ya uzazi.
Kuhusu Familia Kitchen Party Gala, Mratibu wa Jukwaa hilo, Vida Mndolwa kutoka Asasi ya Women in Balance alisema Jumapili ni zamu ya wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kufanyika kwa mafanikio makubwa katika mikoa ya Dodoma na Mwanza ambapo zaidi ya wanawake 600 walipima afya zao.
Alisema kupitia jukwaa hilo, wanawake watapata nafasi ya kupewa elimu ya kitaalamu kuhusu uzazi wa mpango, Ukimwi, malaria, ndoa, malezi ya watoto, ujasiriamali na watapata nafasi pia ya kubadilishana mawazo kwa lengo la kupanua saikolojia na ufahamu wao.
Akizungumzia jukwaa hilo, Mratibu wa Mawasiliano wa PSI Kanda ya Mashariki, Mohammed Mziray alisema shirika hilo limekuwa linafanya kazi na wadau wengine ikiwemo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika kuboresha afya za wanawake kwa lengo la kupunguza vifo vya akina mama na watoto.
Alisema kutokana na mkakati huo ndio maana shirika hilo limeamua kushirikiana na Asasi ya Women  in Balance ili kuendesha jukwaa la Familia Kitchen Party Gala ambalo linawawezesha wanawake kutumia mikusanyiko ambayo ilikuwa imezoeleka kwa mafunzo ya ndoa tu, kuwapa pia elimu ya afya ya uzazi, Ukimwi, malaria na ujasiriamali kwa kuwatumia wataalamu mbalimbali.

No comments: