MJUMBE ATAJA MAKABILA YA BARA YALIYOKUTWA ZANZIBAR

Wakati hoja za kubatilisha Muungano uliodumu kwa miaka 50 sasa zikizidi kupoteza nguvu, Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Riziki Said Lulida, ameonya Watanzania kuacha kubaguana kwa misingi ya upande wa Muungano kwa kuwa wao ni ndugu wa damu.
Kwa mujibu wa Lulida, asilimia zaidi ya 95 ya Wazanzibari, wanatoka Tanzania Bara na walifika Zanzibar kabla ya Uhuru wa Tanganyika, Mapinduzi ya Zanzibar na Muungano wa mwaka 1964.
Akichangia mjadala wa rasimu ya Katiba kuhusu sura ya kwanza na ya sita juzi, Lulida huku akitoa historia ya asili ya wenyeji wa Zanzibar, alisema hakuna Mzanzibari anayeweza kujitoa kuwa hana asili ya Tanzania Bara na kama yupo, basi huyo ni mlowezi na si Mtanzania wa Zanzibar kwa asili. 
“Huwezi kuikwepesha Zanzibar na historia ya Kilwa, wakati huo Sultani wa Oman mwaka 460 AD na Washirazi walienda Kilwa wakaweka makazi yao Pwani yote, kuanzia Mombasa mpaka Kilwa yote,” alieleza Lulida.
Alisema kati ya Washirazi hao, kulikuwa na ndugu wawili aliowataja kuwa ni Ali bin Hassan na Muhibu bin Hassan, ambao walifanya biashara ya meno ya tembo na dhahabu na baadaye mwaka 1505, aliyekuwa Mfalme wa Kilwa wakati huo aliondolewa na kukimbilia Zanzibar na wafuasi wake.
Lulida alisema wakiwa Zanzibar, walikuta makabila ya kwanza ya eneo hilo ambayo ni pamoja na Wayao, Wamwera, Wamakonde, Wangindo na Wandengereko na hapo biashara ya utumwa kutoka Bara kwenda Zanzibar, ilifanyika huku Zanzibar ikijulikana kama Visiwa vya Wavuvi.
Kwa mujibu wa Lulida, mmoja kati ya ndugu hao wawili,  alikimbilia Pemba ya Msumbiji na mwaka 1513 aliondolewa na kukimbilia Pemba huku vita ya Wareno ikimpeleka mwingine Zanzibar.
Alisema majina yote ya koo zinazopatikana Pemba na Unguja, asili yake ni makabila ya Bara ambapo aliyataja majina  yao na asili yake kwenye mabano kuwa ni pamoja na Usi (Yao), Faki na Makame (Makonde), Mfaranyala na Moyo (Ngoni), Natepe na Nahodha (Ngindo), Shamte na Kaojole (Ndengereko) na Masauni (Matumbi).
Lulida alisema Washirazi na wageni wengine weupe, walizaliana na watu weusi wa eneo hilo na kwamba asili ya Zanzibar ni vizazi vya watu weusi kutoka Bara, hivyo si sawa Mzanzibari mweupe kumuona mwenzake mweusi kuwa si Mzanzibari.
Alisema uwepo wa historia hiyo, unadhihirisha wazi kuwa, Zanzibar imetokana na watu wa Bara kwa asili hivyo kuvunja Muungano au kuuweka hatarini, ni kuhatarisha maisha ya  ndugu wa damu wanaodhihirishwa na historia hiyo.
Wakati Bunge hilo lilipoanza baadhi wa wajumbe wake kutoka kundi walilojiundia la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), bila kujali undugu huo wa damu wa Muungano, walidai  Hati ya Muungano haipo, na hivyo kukosekana kwake kunabatilisha Muungano huo huku wakiwakashifu waasisi wake, Mwalimu Julius Nyerere na Shekhe Abeid Amaan Karume.
Wajumbe hao, kupitia msemaji wao Tundu Lissu, walidai kuwa waasisi hao waliongoza Tanzania katika Muungano uliodumu kwa miaka hamsini ya uongo na udikteta na kauli zingine za kuwakejeli.
Hoja nyingine walizojenga kutaka kubatilisha Muungano, ni kwamba hakuna Sheria inayoonesha Baraza la Mapinduzi, liliridhia Muungano na hivyo kuna uwezekano Muungano haukuridhiwa Zanzibar, isipokuwa ipo Sheria inayoonesha Bunge la Jamhuri ya Muungano kuridhia kwa upande wa Tanganyika.
Hata hivyo, Serikali iliamua kutoa Hati ya Muungano iliyosainiwa na waasisi hao ambayo iliwaumbua wajumbe wa Ukawa, wakaamua kuja na hoja kwamba huenda imeghushiwa kwa madai watu wengi walitaka kuiona bila mafanikio.
Juzi Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Dk Harrison Mwakyembe, alisema mjadala wa uhalali wa Hati ya Muungano kisomi ulifungwa miaka ya 1990.
Akifafanua sababu ya kufunga mjadala huo, Dk Mwakyembe alisema Tume ya Nyalali, ilikaa chini na kuzungumza nawajumbe wawili waliokuwepo katika Baraza la Mapinduzi, Profesa Abrahman Babu na Khamis Ameir, ambao walithibitisha kuwa waliridhia Muungano.
Sababu nyingine ya kufunga mjadala huo kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, ni ya kisheria ambayo imeweka wazi kuwa uwepo wa Muungano kwa miaka 50 unaupa uhalali hata bila ya kuwepo kwa Hati ya Muungano.
“Tunashangaa sasa hawa vijana waliozaliwa juzi wametoka wapi,tunapoteza muda kujadili vitu ambavyo havina mantiki tena vilishapitishwa,  sijui hawasomi?” Alihoji Dk Mwakyembe.
Alifafanua kwamba hata kama Baraza la Mapinduzi halikuridhia Muungano huo, uwepo wake kwa karibu miaka 50 sasa, hata Profesa Costa Mahalu na Dk Asha Rose Migiro, ambao  wamezamia katika fani ya sheria, wanajua kisheria kuwa muda huo wa miaka 50 ya Muungano, umeupa uhalali hata kama kusingekuwepo na Hati ya Muungano.
“Hati hizo zimeshakuwa halali, kwanza walikuwa wapi mudawote huo wasidai? Wanakumbuka shuka kumeshakucha?” Alisema Dk Mwakyembe.

No comments: