IDA YAPIGA JEKI UJENZI WA RELI YA KATI

Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia imeidhinisha msaada wa dola za Marekani milioni 300 kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo (IDA) kwa ajili ya kuongeza nguvu jitihada za Serikali katika mradi wa ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya reli.
Katika mradi huo, Tanzania inatarajia kujenga reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam-Isaka pamoja na kuimarisha wakala zinazosimamia reli nchini humo, ikiwa ni sehemu ya mradi wa korido ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa Tanzania, Philipe Dongier, mradi huo ni muhimu kwa Tanzania kutokana na ukweli kuwa nchi hiyo, imebarikiwa hasa eneo ilipo, madini, maliasili za kilimo, utalii na umuhimu wake katika usafiri wa maji hasa kwa nchi zisizozungukwa na maji.
“Sifa hizi zinaipatia fursa Tanzania ya kujiwekea maendeleo mazuri ya kutoa huduma kupitia miundombinu ya kisasa, tuna hamasa kubwa ya kuisaidia juhudi za Serikali katika kujenga upya mfumo wa kisasa wa miundombinu ya reli,” alisema Dongier.
Alisema mradi huo, pia unatarajiwa kuimarisha soko la mazao ya kilimo, kutengeneza ajira, kuisogeza karibu Tanzania na nchi za jirani kwa kuimarisha shughuli za kijamii na kiuchumi lakini pia kuboresha usafiri huo ambao ni tegemeo la wananchi hasa wenye kipato cha chini.
Akizungumzia fedha hizo zilizoidhinishwa, mkurugenzi huyo alisema zitasaidia katika  mradi huo kuanzia ujenzi wake hadi uendeshaji wa treni, kuboresha uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam na vituo vya treni.
“Fedha hizi zitaboresha njia za treni kuwa za kisasa, kujenga vituo vya treni kwa mtindo wa kisasa, kukarabati na kujenga upya maeneo ya madaraja,” alisisitiza.
Alisema kutokana na hali ya sasa ya miundombinu nchini humo na maeneo mengi ya Afrika Mashariki, shughuli za kiuchumi zimekuwa zikisuasua na kusababisha usafirishaji wa bidhaa kuwa wa gharama kubwa baina ya Tanzania na nchi jirani kama vile Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.
Kwa upande wake, kiongozi wa timu ya benki hiyo maalumu kwa ajili ya mradi huo, Henry des Longchamps, mradi huo utasaidia kuboresha na kuunganisha mawasiliano ya usafiri muhimu kwa Tanzania na nchi za jirani na kutengeneza ushindani wa kibiashara na nchi nyingine za jirani zenye miundombinu bora.

No comments: