IMF YASISITIZA UTHABITI BRN KUPUNGUZA UMASIKINI

Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limesema Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) iwapo utatekelezwa kikamilifu  katika sekta kadhaa, utasaidia upatikanaji wa ajira na kupunguza umasikini nchini.
Shirika hilo limebainisha katika ripoti yake kuwa, ukuaji wa uchumi wa Tanzania utasaidia  kuondoa  umasikini pale kutakapokuwa na sera madhubuti zitakazochochea kuboresha sekta ya kilimo pamoja na kujenga viwanda vitakavyopunguza tatizo la ajira nchini.
Ripoti hiyo ya IMF ya uchumi kwa nchi za ukanda wa kusini mwa Jangwa la Sahara, imesisitiza kuwa ili Tanzania iweze kuwakwamua  watu wake katika lindi la umasikini, ni lazima iwekeze zaidi kwenye elimu kwa kuhakikisha kuwa inakuwa na sera nzuri zitazosaidia kuboresha sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na miundombinu yake.
Ofisa Mkazi wa IMF nchini, Thomas Baunsgaard akiwasilisha ripoti hiyo  katika mkutano ulioandaliwa na Asasi ya Utafiti wa Uchumi (REPOA), alisema  uchumi wa Tanzania umekua kwa asilimia saba, lakini hata hivyo kukua huko hakujasaidia kupunguza umasikini miongoni mwa wananchi wake.
Akichangia kwenye ripoti hiyo, Profesa Ibrahim Lipumba alisema  ripoti hiyo inasaidia Tanzania kubuni sera za kuboresha uchumi wake na akashauri misamaha mingi ya kodi iondolewe kwani inachangia upotevu wa asilimia tano ya pato la taifa kwa mwaka.
Mkurugenzi wa Utafiti wa REPOA, Dk Donald Mmari alisema matumizi ya Serikali ni makubwa kuliko kiasi kinachokusanywa, jambo ambalo alisema linachangia kuwepo kwa mfumuko wa bei na hivyo kuwaathiri wafanyakazi.

No comments: