HATI YA MUUNGANO HII HAPA, SASA KUHIFADHIWA MAKUMBUSHO YA TAIFA

Hatimaye baada ya upotoshwaji mkubwa wa baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, hasa waliojiundia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kuwa Hati ya Muungano haipo, sasa Serikali imeweka hati hiyo hadharani.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema kuwa Rais Jakaya Kikwete ameridhia hati hiyo ioneshwe na waandishi wa habari walikuwa wa kwanza kuiona hati halisi jana.
Hati hiyo ambayo mwandishi aliiona, imepigwa chapa na taipureta na ina kurasa tatu na jalada lake lina rangi ya damu ya mzee.
Aidha, ili kuondoa upotoshwaji wa makusudi uliofanywa na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba hasa kutoka Ukawa, Balozi Sefue alisema Rais Kikwete ameridhia nakala zilizothibitishwa, ziwekwe kwenye Makumbusho ya Taifa ili kila mwananchi aione na kuepuka upotoshaji huo.
Alipoulizwa kama Hati hiyo pia ipo Umoja wa Mataifa, Balozi Sefue alisema: "UN wasingeweza kuondoa kiti cha Tanganyika na Zanzibar kama kusingekuwapo hati ya makubaliano ya kuwa nchi mbili zimeungana na kuwa Tanzania."
Alipoulizwa ni kwanini Serikali ilichelewa kutoa hati hiyo na ni wapi inahifadhiwa, Balozi Sefue alisema; "inatosha kuwahakikishia wananchi kuwa hati zote tatu zipo salama, na kutokana na teknolojia zilizotumika, hati hizo hazitolewi ovyo."
Alisema kuchelewa kuitoa kunaweza kuwa kosa kwa kuwa hawakutarajia upotoshwaji kufikia ulipofikia, lakini akasisitiza kuwa hawezi kusema inapohifadhiwa.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliliambia Bunge jana kuwa tayari ametumiwa na Ikulu, nakala ya Hati ya Makubaliano ya Muungano iliyosainiwa na Mwalimu Nyerere na Abeid Karume.
Alisema kutokana na hatua hiyo, alimkabidhi Mwenyekiti wa Bunge Maalumu Samuel Sitta nakala hiyo, wakati Bunge  hilo likisubiri hati iliyothibitishwa kisheria itakayowasilishwa katika Bunge hilo ndani ya siku mbili kati ya leo na kesho.
Akizungumzia hatua hiyo, Sitta alisema itakapowasili hati iliyothibitishwa kisheria, ataitoa nakala na kusambaza kwa wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba ili waisome na kuwasaidia katika kujenga hoja za majadiliano bungeni.
Akizungumzia ilipokuwa hati hiyo, Balozi Sefue alisema hati hiyo ipo, ilikuwepo siku zote na kufafanua kuwa ni lazima baadhi ya hati muhimu zihifadhiwe kama mboni ya jicho.
"Lazima tukubaliane kuwa zipo hati fulani ambazo ni kiini cha uwepo wetu kama Taifa huru, Jamhuri huru na Muungano huru, ambazo tunazihifadhi kama mboni ya jicho.
"Hati hizo ni pamoja na Hati ya Uhuru wa Tanganyika ya mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962, na Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964. Hati za aina hii zinahifadhiwa maeneo maalumu ambayo ni salama ili zisipotee wala kuharibika. Kwa kawaida hatuzitoi, tunazifungua ili kuzihifadhi kwa namna yoyote ile," alisema Balozi Sefue.
Kwa kuwa upotoshwaji huo usiotarajiwa umefanyika kwa nguvu katika Bunge Maalumu la Katiba, Balozi Sefue alisema kama Bunge Maalumu likiomba nakala halisi, kama hawataridhika na nakala zilizothibitishwa, ombi hilo litafikishwa kwa Rais Kikwete na akiridhia, itapelekwa wakaione.
"Na, tukiombwa kufanya hivyo na Mwenyekiti wa Bunge Maalum, nina uhakika Rais ataridhia ipelekwe huko ili kuondoa mjadala wa kama Hati ipo au la.
"Isitoshe, tufanye utaratibu wa kuweka nakala kwenye Makumbusho ya Taifa, ili kila atakayetaka kuiona katika miaka mingine 50 ijayo na kuzidi, aione," alisema Balozi Sefue.
"Sasa maneno yamekua mengi, tuhuma zimekuwa nyingi, dhihaka zimekuwa nyingi, kiasi cha wananchi kuanza kutiwa mashaka iwapo kweli Hati ya Muungano ipo au la.
"Hivyo, kwa maagizo na ridhaa ya Mheshimiwa Dk Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ninaleta mbele yenu Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliyotiwa saini Zanzibar na waasisi wetu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amaan Karume.
Aliendelea kusema lengo ni; "Ili muione na kuwahakikishia Watanzania kuwa yanayosemwa kuwa hakuna Hati hiyo si kweli.
Hati hiyo ipo tangu wakati huo, imetunzwa vizuri na waliotutangulia, tumeirithi, na tutaendelea kuihifadhi."
Balozi Sefue aliendelea kueleza masikitiko ya Serikali, kwamba leo, miaka 50 baada ya Mungano, kumeibuka dhana potofu inayojengwa kuwa Muungano huu si halali kwa vile hakuna Hati ya Muungano.
Alisisitiza kuwa kwa upande wa Serikali wamesikitishwa na kufadhaishwa sana na tuhuma nzito kwamba labda waasisi   hawakuwa makini au walifanya kiini macho na kusema hawakutarajia wawepo Watanzania wenzao wafikie hapo.
"Ni jambo zito. Vile vile hatukutarajia kuwa Serikali itatuhumiwa kuwa haikuwa makini kuhifadhi walichosaini waasisi wetu.
"Waasisi wa Taifa letu ambao tarehe 22 Aprili, 1964 kule Zanzibar walitia saini Hati hiyo, mbele ya mashuhuda, nao wameonekana kama walichokifanya kilikuwa kiini macho, na kwa hiyo kwamba waliongoza Taifa jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msingi wa kiini macho hicho kwa miaka yote hadi Mwenyezi Mungu alipowaita.
"Mambo yote mawili yametusononesha sana sisi serikalini, na bila shaka yamewasononesha wananchi wanaoipenda nchi yao, wanaowapenda waasisi wa Taifa letu na kuuenzi Muungano wao," alisema Balozi Sefue.
Alifafanua kuwa madai ya kuoneshwa Hati ya Muungano yalianza siku nyingi, lakini Serikali haikuamini kwamba hali ingefikiwa ilipofikia, ambapo watu wamethubutu kudai na kuapa kuwa hati hiyo haipo.
"Matumaini yetu ni kuwa baada ya leo (jana) tutaendelea na mambo ya msingi kwa mustakabali, umoja na uimara wa Taifa letu badala ya kuchochea hisia kuwa Muungano wetu hauna msingi imara wa kisheria," alisema.
Sehemu kubwa ya upotoshaji ulisambazwa kwamba hakuna Hati za Muungano, ulilenga kubatilisha Muungano uliodumu kwa miaka hamsini sasa, ili hoja ya kubadilisha muundo wa Muungano kutoka kuwa serikali mbili kwenda serikali tatu ipate nguvu.
Waliokuwa wakidai kuwa hati hizo hazipo, hasa kutoka kundi la  Ukawa, walitumia namna mbalimbali za kufuta uhalali wa Muungano.
Wakati kamati za Bunge Maalumu la Katiba zilipoanza kukaa na kujadili Rasimu ya Katiba, hoja ya kwanza ya wajumbe hasa kutoka Ukawa, ilikuwa Hati ya Muungano  iliyotiwa saini na waasisi wa Muungano, Mwalimu Nyerere na Shekhe Karume  iwasilishwe waione.
Wajumbe hao walipewa nakala ya Sheria ya Kuridhia Muungano iliyotiwa saini na Mwalimu Nyerere na aliyekuwa Katibu wa Bunge wakati huo, Pius Msekwa.
Hata hivyo, baadhi ya wajumbe hasa kutoka Ukawa unaoundwa na vyama vya upinzani ukiongozwa na CUF na Chadema, walidai sahihi zilizoko katika hati hizo, zimeghushiwa.
Kutokana na utata huo, Kamati namba 2 ya Bunge Maalumu la Katiba, ilimuita Msekwa kutoa ufafanuzi kuhusu hati hizo, na akasisitiza kuwa sahihi hizo ni halali.
 Mwenyekiti wa kamati hiyo, Shamsi Vuai Nahodha, alithibitisha   kwamba walilazimika kumuita Msekwa ili kupata ufafanuzi wa masuala kadhaa.
Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Hamis Hamad naye alisema hati hiyo ipo Dar es Salaam na ni moja tu, hivyo siyo rahisi kupelekwa bungeni Dodoma.
"Ile hati ya Muungano ipo Dar es Salaam, lakini tunahofia kuileta maana inaweza kupotea kwani ipo moja tu, sasa ambacho tutakifanya inaweza kutolewa nakala na kuthibitishwa na mawakili na ikaja nakala hapa Dodoma iwapo wajumbe wanahitaji," alisema Hamad.
Baada ya majibu hayo, wajumbe hao waliendelea kutafuna namna ya kubatilisha Muungano, ambapo walisema Sheria Namba 22 ya 1964 ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar kuridhia Muungano nayo haijulikani ilipo.
Wajumbe hao walikiri kuwa Bunge la Tanganyika ushahidi wameletewa kuwa waliridhia Muungano Aprili 25, 1964 na waliosaini ni Julius Nyerere, Katibu wa Bunge hilo, Pius Msekwa na aliyekuwa Spika Adam Sapi Mkwawa, lakini kwa Zanzibar haupo.
Walidai wa kuwa kitendo cha Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman kusema hajawahi kuiona sheria hiyo, kinadhihirisha kuwa haipo.
Pamoja na Msekwa kukiri kwenye kamati hiyo kuwa saini iliyopo kwenye hati ya makubaliano ya Muungano ni yake, lakini wajumbe hao waliendelea kudai si yake na imechezewa.
Wajumbe walihoji tofauti baina saini iliyopo kwenye sheria hiyo na saini yake katika nyaraka nyingine rasmi.
Wajumbe walioibua hoja hiyo wakiongozwa na Godbless Lema, pia walitilia shaka matumizi ya kompyuta katika sheria hizo zilizoandikwa mwaka 1964.
"Mwaka 1964 hakukuwa na kompyuta lakini hapa tunaona sheria zimeandikwa kwa kompyuta na hata sehemu ya saini ya Msekwa na Nyerere kuna herufi zimeandikwa kwa kompyuta," alinukuliwa Lema.
Katika maelezo yake Msekwa licha ya kukiri upungufu, aliwakumbusha wajumbe kuwa siku ya kusainiwa hati hizo, picha zilipigwa na zipo hadi sasa.
Hata Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Sitta alisema anahisi sahihi zimechezewa baada ya kufutika, lakini sheria hiyo ni halisi na iliwekwa sahihi na Mwalimu Nyerere, Spika Mkwawa na Msekwa.

No comments: