SERIKALI YATOA TAMKO KUHUSU BOMU LA ARUSHA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe amesema watu 12 wamejeruhiwa baada ya kulipuka kwa bomu katika Klabu ya Usiku ya Night Park jijini Arusha.
Akitoa taarifa ya serikali Bunge Maalum la Katiba jana, Chikawe alisema maofisa wa uchunguzi wametumwa jijini Arusha ili kuchunguza tukio hilo ambalo amesema halijasababisha vifo.
Alisema mtu mmoja asiyefahamika alifika katika Klabu hiyo usiku jana akiwa na mfuko wa plasitiki ndani akiwa ameweka bomu hilo na alipofika katika klabu hiyo alilitoa na kuwasha utambi na yeye kuondoka na muda mfupi baadaye likalipuka.
Alisema mbali ya kitendo hicho, mtu huyo alikwenda katika baa nyingine ya Washington na kutoa bomu jingine kama hilo na kuwasha utambi lakini kwa bahati nzuri bomu hilo halikulipuka.
"Tunaendelea kufanya uchunguzi wa kina kwa suala hili ili kujua mtu huyo ni nani na malengo yake yalikuwa yapi," alisema Chikawe.
Hata hivyo alipotaka kutoa ufafanuzi wa ndani zaidi kwa tukio hilo, Chikawe alikumbana na upinzani kutoka kwa wajumbe , ambapo Mjumbe Charles Mwijage alisema ni hatari kwa usalama wa nchi kulieleza suala
"Mheshimiwa Mwenyekiti (Samuel Sitta) itoshe tu kwa mtoa taarifa (Chikawe) kutoa taarifa lakini kuingia kwa undani kueleza namna bomu hilo la kienyeji lilivyotengenezwa ni hatari kwa usalama wa nchi," alisema Mwijage.
Wakati huo huo Mmoja wa majeruhi 11 waliolazwa Hospitali Mkoa  ya Mount Meru Jijini Arusha, Obed Mbasha alisimulia yaliyomkuta baa  ya Arusha Night Park eneo la Mianzini akiangalia mpira wa ligi ya Ulaya.
Alisema alisikia kitu chenye mlio mkali huku watu wengine wakikimbia wakisema bomu bomu na akajikuta ghafla hawezi kukimbia mbali kutokana na maumivu aliyokuwa akiyasikia kwenye mguu wake wa kulia.
"Nashukuru Mungu japo nina majeraha lakini napumua nilisikia mlio mkubwa na watu wanakimbia,  nilijaribu kukimbia nikashindwa ndipo nilipojikuta nipo chini hata sijui nilivyokuja," alisema.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Frida Mokiti alisema walipokea majeruhi 17.  Kati ya hao, 11 wamelazwa hospitalini hapo. Watano waliruhusiwa baada ya kupatiwa matibabu na mmoja amelazwa hospitali ya Selian. Alisema mmoja hali yake si nzuri na inatarajiwa kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili.
Alitaja majina ya majeruhi wanane ni  Christian Mmasi, Ally Sudi, Evarest Kaaya, Evance Maleko, Pius Shayo, Peter Mkereme, Obed Mbasha na Anterius Mganda.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo  alifika eneo la tukio la bomu na pia kutembelea wagonjwa.
Mkurugenzi wa baa hiyo, Joseph Karugendo alisema  wafanyakazi wake saba ni miongoni mwa majeruhi wa tukio hilo na kusema  bomu hilo limepigwa katikati ya mlango mkuu wa kuingia.
Alisema hawana shaka ya kumpata mhusika aliyefanya tukio hilo kwani ndani ya baa hiyo wamefunga mitambo ya kamera ya CCTV. Kwa mujibu wake, baada ya tukio polisi walizingira mtambo huo kuhakikisha hauvurugwi na unalindwa hadi jana.

No comments: