BENKI YA POSTA YATENGA SHILINGI MILIONI 150 KUSAIDIA JAMII

Benki ya Posta Tanzania (TPB) imesema imeandaa Sh milioni 150 kwa ajili ya miradi  ya kusaidia jamii.
Mkurugenzi wa benki hiyo, Sabasaba Moshingi alisema hayo jana akizungumza na waandishi kuhusu mafanikio waliyoyapata kwa mwaka 2013.
Alisema mwaka jana iliandaa Sh milioni 100 kusaidia jamii  kupitia miradi mbalimbali  zikiwemo shule.“Tunashukuru kuona benki yetu imekuwa karibu sana na jamii na tuliweza kujenga shule ya Misungwi iliyopo Mwanza natulikarabati madarasa na kununua madawati, ”alisema Moshingi na kwamba mwaka huu imeongeza kufikia Sh milioni 150.
Akizungumzia mafanikio zaidi, alisema mwaka jana wamepata Sh bilioni 6.99 kabla ya kodi kutoka Sh bilioni 5.6 za mwaka juzi. Ukuaji huo ni asilimia 24.
Benki hiyo imesema imeboresha matawi yake ikiwemo tawi la Morogoro, Manzese na Kigoma. Matawi madogomadogo  ya Tegeta na Chakechake Pemba pia yanakarabatiwa. 
“Ukuaji wa matawi unaleta wateja wapya na mpaka mwishoni mwa mwaka 2013  tulikuwa na  wateja 670,000,” alisema.
Alisema mwaka huu wamejizatiti kuendelea kutoa huduma bora, nafuu na za kisasa ikiwemo huduma ya TPB popote inayofadhiliwa na Melinda and Bill Gates Foundation.
Kupitia huduma hiyo, benki maana wanaweza kupata huduma hizo kutumia simu zao za mkononi na vilivile kupata huduma zote za kibenki kupitia mawakala ambao sasa ni zaidi ya 160 nchini Tanzania.
Pia benki imeungana na makampuni ya simu Vodacom, Airtel na Tigo ambapo wateja wa benki ya Posta wanaweza kutuma pesa kutoka kwenye akaunti zao kwenda akaunti zao za Airtel money, M-pesa na Tigo-pesa pia kutuma pesa kutoka kwenye simu zao kwenda kwenye akaunti zao za benki.
“Tunaamini kwamba bado kwa kutumia teknolojia ya TPB POPOTE tutaweza kuwafikia watanzania walio wengi hasa vijijini ambao bado hawajaingia kwenye mfumo wa kifedha,” alisema Moshingi.

No comments: