TWEET BORA ZA DK REGINALD MENGI KUTUNGIWA KITABU

Kitabu kitakachokuwa na mawazo yaliyoshinda kwenye shindano la tweet na Mengi kinaandikwa ili kuwapa fursa Watanzania kusoma na kuyatumia mawazo hayo bora ili kuweza kutambua fursa zilizopo zitakazowawezesha kujiajiri.
Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Dk Reginald Mengi aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kitabu hicho kitaandikwa baada ya shindano hilo kutimiza mwaka mmoja tangu lianzishwe Mei mwaka jana.
"Tunataka kuona mawazo hayo bora yanafanyiwa kazi, naamini yatawasaidia Watanzania wa kawaida kusonga mbele kiuchumi," alisema Dk Mengi wakati wa kukabidhi zawadi kwa washindi wa shindano hilo wa mwezi Machi.
Katika shindano la mwezi Machi la Tweet na Mengi, swali liliuliza toa mfano wa jinsi kitu kinavyokuwa kero kwa watu wengi, lakini kinaweza kugeuka kuwa fursa ya  kibiashara. Jumla ya Tweet 1,935 zilitumwa kujibu swali hilo.
Dk Mengi alisema mawazo yaliyotolewa mengine hayahitaji mitaji mikubwa, bali yanahitaji ubunifu wa mtu mwenyewe wa namna ya kuyatumia mawazo hayo. Mengi alisema tatizo la ajira ni kubwa nchini hivyo kila juhudi zinatakiwa kuhakikisha kila mtu anatoa mchango wake kuhakikisha vijana wanasaidiwa katika eneo hilo.
Katika shindano la mwezi Machi, Mshindi wa kwanza aliyejinyakulia Sh milioni moja ni Gerald Nyaissa ambaye katika wazo lake alisema mikoa ya Dodoma na Iringa ina upepo mkali mpaka kero, hivyo akashauri vijana waanzishe miradi ya kufua nishati ya umeme kwa kutumia upepo.
Glory Ndewario mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi alikuwa mshindi wa pili na akapata Sh 500,000. Katika wazo lake, alisema kero ya misongamano katika miji ni sehemu za manunuzi, hivyo watu watumie fursa hiyo kuanzisha biashara ya kufanya manunuzi kwa niaba ya watu kwa malipo.
Mshindi wa tatu katika shindano hilo ambaye alijinyakulia Sh 300,000 ni Mkuu wa Shule ya Itemba iliyoko Babati mkoani Manyara Polycarp Mramba ambaye alisema ukataji miti misituni kwa ajili ya kuni, mkaa na matumizi mengine  ni kero, unaweza kutafuta mbegu za miti upande kisha uuze kwa bei nafuu. 
Swali la mwezi Aprili linahoji mzazi afanyeje nini kumwandaa mtoto kufanikiwa kiuchumi?

No comments: