HOSPITALI YA AGA KHAN YAZINDUA KITUO CHA SARATANI

Hospitali ya Aga Khan imezindua kituo cha matibabu ya saratani jijini Dar es Salaam ikiwa ni katika maadhimisho ya miaka 50 tangu hospitali hiyo ilipoanza kutoa matibabu nchini.
Hospitali hiyo pia imejipanga kusogeza huduma zao za matibabu ya saratani kwa wananchi kutokana na maeneo mengi kutokuwa na matibabu ya ugonjwa huo na kusababisha vifo vya baadhi ya wagonjwa.
Hayo yameelezwa na Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Jaffer Dharsee ambaye alisema hospitali hiyo itashirikiana vizuri na serikali ili kuwezesha huduma za matibabu ya saratani kupatikana, kutokana na vituo vya matibabu ya maradhi hayo  kuwa mbali hivyo ugonjwa kugunduliwa wakati uko katika hatua ya mwisho.
Aidha, alisema wametenga kiasi cha dola za Marekani milioni 80 ambazo zitatumika katika mambo mbalimbali ya kuboresha huduma ikiwa ni pamoja na kuwasomesha wauguzi wao na kutanua huduma nje ya hospitali kwa kuongeza vitengo vya matibabu hasa katika mikoa ambayo tayari inatoa huduma hiyo kama Kilimanjaro, Arusha na Mwanza.

No comments: