AZAKI YADAI MIJADALA BUNGE MAALUMU IMEPOTEZA UTAIFA

Umoja wa Asasi za Kiraia (AZAKI) nchini umeelezea masikitiko yake kuhusu mijadala inayoendelea ndani ya Bunge Maalumu la Katiba ambayo imepoteza utaifa na badala yake imejikita katika kutoheshimiana, ubabe, ubaguzi, vijembe na vitisho.
Mwenyekiti wa asasi hiyo, Irinei Kiria amesema umoja huo haujafurahishwa na malumbano yasiyo na tija  yanayochukua muda mrefu kwenye mambo madogo na kupelekea kupoteza muda na hivyo kutumia rasilimali za umma vibaya.
Kiria ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akitoa tamko la umoja huo kwa waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa mchakato wa kutunga katiba mpya unaoendelea mjini Dodoma.
Alisema tathmini yao imeonesha taswira iliyopo sasa hasa katika Bunge Maalumu la Katiba inafifisha  matarajio ya wananchi kupata Tanzania mpya, kwa kuwa haioneshi dalili zozote nzuri za kupata katiba ya wananchi.
Kiria amesema mwenendo mzima wa Bunge Maalumu la Katiba umechukua sura ya ubinafsi na yenye maslahi ya kivyama zaidi na kusahau maslahi ya Watanzania na mustakabali wa Taifa.
Tunasikitishwa kwamba mjadala unaoendelea kule bungeni unaondoa matumaini ya Watanzania kupata katiba bora na zaidi linazidi kuwatenganisha Watanzania badala ya kuwaunganisha kama ilivyotarajiwa.
AZAKI imemwomba Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta kuchukua hatua zaidi kwa wale wanaotoa vitisho, matusi na lugha za ubaguzi kwa baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba na Watanzania kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba ameshauri Bunge hilo Maalumu la Katiba likavunjwa na kuanzisha utaratibu mwingine wa kuunda bunge jingine kutokana na lililopo kushindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

No comments: