EAC YAKIRI MAKOSA KUITENGA TANZANIA KWENYE VIKAO

Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimekiri kuwa zilikosea kuitenga Tanzania katika mikutano ya jumuiya hiyo na kwamba hali hiyo haitajirudia.
Imesisitiza kuwa, kukutana kwa nchi wanachama na kuzungumza mambo yasiyo ya jumuiya si vibaya, bali ubaya unakuja zinapotengwa baadhi ya nchi ilhali kinachojadiliwa kinakuwa cha jumuiya yote.
Hayo yalisemwa jana mjini hapa na Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama wa Wizara hiyo, Steven Mbundi wakati wa kongamano la Mtangamano wa jumuiya hiyo ambayo baadhi ya wadau walielezea kuonesha wasiwasi wa kuvunjika kwake kutokana na Tanzania kutengwa katika baadhi ya vikao.
"Hofu ilianza baadhi ya nchi zilipokutana na kuanza kujadili masuala ya jumuiya bila kuwepo nyingine kama utungaji wa Katiba, lakini kwa sasa tumezungumza na yote yamesimama na kukubali kuwa walikwenda kinyume na taratibu," alisema Mbundi.
Mwaka jana,  iliibuka hofu ya baadhi ya mshikamano wa nchi wanachama wa EAC baada ya Tanzania kutengwa katika vikao kadhaa zilivyofanyika kwa awamu katika baadhi ya nchi hizo.
Mbali ya Tanzania, nchi nyingine wanachama wa EAC ni Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda.

No comments: