ANNA ABDALLAH ATAKA WANAOTUKANA WAASISI WAPIMWE AKILI

Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Anna Abdallah amesema mtu yeyote anayewatukana waasisi wa Taifa, anapaswa kupimwa akili.
Alisema kuwakashifu waasisi ni sawa na kuwakashifu wazazi waliokuzaa na mtu anayefanya hayo, ana upungufu fulani katika akili yake.
Abdallah aliyasema hayo bungeni mjini hapa alipokuwa akichangia mjadala wa Rasimu ya Katiba, kuhusu Sura ya Kwanza na ya Sita baada ya kamati 12 za Bunge hilo kuwasilisha ripoti zao.
“Hapa tumeletwa na Taifa kuandika Katiba ya wananchi, Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi), wangesema kwamba wao wanataka Katiba ya wachache tungeelewa maana sasa Watanzania wameelewa, maana wametulia na kutusikiliza hoja zetu,” alisema Abdallah.
Alisema yaliyofanyika ndani ya Bunge ingekuwa ni nje, watu wangepigana lakini kwa kuwa kuna kinga, watu wamesema wanavyotaka lakini si sahihi kuwakashifu waasisi wa Taifa.
“Napinga kuwakashifu waasisi wetu, ni sawa na kutukana wazazi waliokuzaa, hata kama walifanya makosa, huwezi kuwatukana, anayetukana anapaswa kupimwa akili,” alisema mjumbe huyo.
Katika mjadala wa Bunge Maalumu la Katiba, wajumbe kadhaa wa Ukawa walikaririwa wakiwakashifu waasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais Abeid Amaan Karume kuwa ni waongo, walikuwa madikteta, jambo lililokemewa na wajumbe wengi kabla na baada ya kundi hilo kutoka bungeni wiki iliyopita.

No comments: