KESI DHIDI YA WAFANYAKAZI 14 WA BENKI YA EXIM YASUASUA

Kesi inayowakabili wafanyakazi 14 wa benki ya Exim tawi la jijini Arusha kwa tuhuma za kuibia benki hiyo zaidi ya Sh bilioni 7.6, inaendelea kusuasua.
Hali hiyo inatokana na madai kuwa uongozi wa juu wa benki hiyo, haujawasilisha kwa wakati ripoti ya ukaguzi wa mahesabu kwa Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Arusha ili kuipeleka mahakamani kwa ushahidi zaidi.
Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi mkoani Arusha na kuthibitishwa na Wakili wa upande wa benki ya Exim, Albert Msando, zilisema Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Arusha,  imeshaiandikia barua tatu benki hiyo makao makuu, kutaka ripoti ya ukaguzi, lakini,  jitihada hizo zimekuwa zikigonga mwamba kila mara.
Taarifa za kipolisi zinasema kukosekana kwa ripoti hiyo, kunakwamisha  kesi hiyo kuanza kusikilizwa,  kutokana na kukosekana ushahidi huo muhimu.
 Vyanzo vya habari kutoka ndani ya jeshi hilo, vilisema ripoti inayohitajika ni ya kutoka mwaka 2008 hadi 2012, muda ambao watuhumiwa hao walikuwa kazini ili Polisi iweze kujiridhisha katika ushahidi wake.
Habari za ndani ambazo gazeti hili linazo zinasema kukwama kwa upatikanaji wa ripoti hiyo ya mahesabu ya miaka 4, kunatokana na hujuma zinazofanywa na baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya Exim waliobaki kazini.
Kusuasua kwa kesi hiyo, kumezua zogo kwa wateja 11 walioibiwa fedha zao katika tawi la Exim Arusha, ambao walivamia ofisi ya Meneja wa benki hiyo jijini Arusha, kutaka kujua hatima ya fedha zao.
Akizungumzia utata huo,  Wakili wa Benki ya Exim, Albert Msando, alikiri Polisi kuiandikia benki hiyo barua zaidi ya tatu za kutaka ripoti ya ukaguzi wa kimahesabu, lakini benki hiyo haijawasilisha mpaka sasa.
 Msando alisema kuchelewa kuwasilisha ripoti hiyo, kunakwamisha kesi kuanza kusikilizwa na pia kumesababisha waombe muda zaidi wa siku 60 ili kukamilisha ripoti hiyo.
Aidha, Msando alikiri kuwepo kwa hujuma zinazofanywa na baadhi ya wafanyakazi waliopo kazini kukwamisha kupatikana kwa ripoti hiyo kwa wakati,  kama njia ya kupoteza ushahidi kwa kesi hiyo.
Akizungumza katika Mahakama ya Mkoa wa Arusha Aprili 23 mwaka huu, Mwanasheria wa Serikali, Haruna Matagane alimweleza Kaimu Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Devotha Kamuzora kuwa ushahidi wa kesi hiyo, bado haujakamilika hivyo aliomba muda zaidi  wa upelelezi, ikiwemo kupatikana kwa ripoti hiyo.
 Kutokana na maelezo ya Mwanasheria huyo, hakimu Kamuzora aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 20 mwaka huu. Alimtaka Wakili wa Serikali kukamilisha upelelezi ili usikilizwaji wa awali uweze kuanza kusikilizwa mara moja.
Wafanyakazi  14 wa Benki ya Exim tawi la jijini Arusha, walifikishwa katika Mahakama hiyo mara ya kwanza Agosti mwaka jana kwa tuhuma ya wizi wa zaidi ya Sh bilioni 7.6  akiwemo Meneja wa benki hiyo, Bimal Gondalia.
 Katika masharti ya dhamana, Hakimu Kamuzora ilitoa amri ya kila mtuhumiwa ,kutosafiri nje ya Mkoa wa Arusha bila idhini ya Mahakama hiyo na kukabidhi hati ya usafiriPpolisi wakati kesi hii ikiendelea.
Mbali na Meneja huyo, washitakiwa wengine ni  Evance Kashebo, Robert Reuben, Tuntufe Aggrey, Joyce Kimaro, Lilian Kageye, Doroth Chijana, Michael Majebele, Ginese Massawe na Joseph Meck. Wengine ni  Livingstone Mwakijabe,Clara Lawena, Neema Kinabo na Christopher Lyimo.

No comments: