WALIMU WAPYA 36,021 KUAJIRIWA APRILI MOSI...

Jumanne Sagini.
Serikali imesema kuanzia Aprili Mosi, mwaka huu itaajiri rasmi jumla ya walimu wapya 36,021, ambao wamehitimu masomo yao mwaka 2013 kutoka vyuo mbalimbali.
Walimu hao watakaoajiriwa rasmi na Halmashauri, walimu wa ngazi ya cheti Daraja la III A ambao hufundisha shule za msingi ni 17,928 na walimu wa shule za sekondari 18,093.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Jumanne Sagini, ilieleza jana kuwa walimu wapya watatakiwa kuripoti kwenye halmashauri walizopangiwa ifikapo Aprili Mosi, mwaka huu bila kukosa ili waanze kazi yao mara moja.
Taarifa hiyo ilisisitiza walimu hao kuwahi ili taarifa zao za kiutumishi zifanyiwe kazi na waajiri wao, kuwawezesha kupata mshahara katika mwezi huo na hivyo kuepuka ulimbikizaji wa mshahara kwa watumishi wapya.
"Kwa vyovyote vile mwalimu yoyote ambaye ataripoti baada ya Aprili 10, mwaka huu bila sababu ya msingi zinazokubalika atakuwa amepoteza nafasi hiyo," ilieleza taarifa hiyo.
Aidha, upangaji wa walimu wapya kwenye halmashauri umezingatia mahitaji ya walimu, huku ikiweka wazi kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi haitafanya mabadiliko yoyote ya vituo vya kufanyia kazi kwa walimu wapya isipokuwa kwa kufuata utaratibu wa kawaida wa uhamisho.
Ilielezwa kuwa ajira zilizotangazwa ni za walimu wapya, hivyo walimu ambao tayari ni watumishi wa umma waliokuwa vyuoni kwa ajili ya kujiendeleza kielimu na wamehitimu mafunzo yao, wanatakiwa kurudi kwa waajiri wao na kuendelea na kazi.
Orodha ya walimu wapya ambayo itaonesha halmashauri walizopangiwa itatangazwa kwenye tovuti ya Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi ambayo ni www.pmoralg.go.tz na ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambayo ni www.moe.go.tz ifikapo Machi 15, mwaka huu.

No comments: