MRAMBA, YONA WAIOMBA MAHAKAMA KWENDA KUTIBIWA INDIA...

Daniel Yona (kushoto) na Basil Mramba.
Aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na Waziri wa zamani wa Nishati na Madini, Daniel Yona wanaokabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya Ofisi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7,  wamewasilisha ombi la kwenda kutibiwa nchini India.
Washitakiwa hao waliwasilisha ombi hilo jana  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro alidai kuwa upande wa Jamhuri hauna taarifa na kuomba washitakiwa kuwapa nakala ya ombi lao ili waandae majibu.
Jaji John Utamwa aliahirisha shauri hilo hadi leo, watakaposikiliza majibu ya upande wa Jamhuri.
Mbali na Mramba na Yona, mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Mipango na Uchumi, Gray Mgonja.
Katika kesi hiyo, washitakiwa wote wanadaiwa kuwa kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14, 2004 jijini Dar es Salaam, wakiwa watumishi wa umma, walitumia vibaya madaraka yao na kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 11.7.
Ilidaiwa kuwa walisababisha hasara hiyo baada ya kutoa msamaha wa kodi kinyume cha sheria kwa Kampuni ya M/S Alex Stewart ya nchini Uingereza.
Tayari Mramba alishajitetea mbele ya Mahakama hiyo, akidai kuwa aliisamehe kodi kampuni hiyo kwa kuwa katika mkataba, walikubaliana kuisamehe kodi.

No comments: