UZINDUZI WA KITUO KIPYA CHA DALADALA UBUNGO WAPIGWA KALENDA...

Kituo kipya cha daladala Ubungo.
Manispaa ya Kinondoni imesitisha mpango  wake wa kukifungua kituo kipya cha daladala, kilichopo  nyuma ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kama ilivyokusudia kufanya  mwezi huu ili kukifanyia mabadiliko kwa kukijenga kwa  kiwango cha lami.
Hayo yalisemwa na Ofisa Habari wa Manispaa hiyo,  Sebastian Mhowera alipokuwa akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho, kinachojengwa kama mbadala wa kituo cha daladala cha Ubungo,  kinachohamishwa ili kupisha ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo kasi chini ya mpango wa DART
Alisema Manispaa ilifikia uamuzi huo ili kuondoa usumbufu, unaoweza kujitokeza hapo baadaye na kuamua kukijenga kituo hicho kwa kiwango cha lami, kama ilivyo kwa kituo cha Mbezi Mwisho, hatua aliyosema itasaidia kukifanya kituo kuwa katika ubora pamoja na mandhari ya kuvutia.
“Matarajio baada ya wiki tano hadi sita ujenzi huo utakuwa umekamilika na hivyo kutoa fursa ya kituo kuanza kazi kama tulivyokuwa tumekusudia, kwa sasa kituo kimejengwa katika kiwango cha changarawe,” alisema Mhowera na kuongeza kuwa fedha za ujenzi huo zinatokana na bajeti iliyopo katika Manispaa hiyo.
Aidha, alisema pamoja na ujenzi huo wa kiwango cha lami wa kituo hicho barabara zinazoingia na kutoka katika kituo hicho, pia kinatarajiwa kujengwa kwa kiwango hicho cha lami ili kuondoa usumbufu kwa daladala hizo na watumiaji wa  kituo hicho.
Alisema huduma zingine zote muhimu katika kituo hicho, ikiwemo ya choo imekamilika na kinachosubiriwa kwa sasa ni kukamilika kwa lami hiyo ili kutoa fursa ya kituo kutumika kikiwa katika hali bora.
Aidha alisema kukamilika kwa kituo hicho, kutatoa fursa ya kuvunjwa kwa kituo cha daladala cha Mwenge ili kutoa fursa kwa mkandarasi anayeijenga barabara iendayo Tegeta, kuendelea na ujenzi katika eneo hilo kutokana na kituo hicho kuwa kikwazo cha ujenzi huo.

No comments: