NICOL YAWAHAKIKISHIA WATEJA WAKE USALAMA WA HISA ZAO...

Felix Mosha.
Kampuni ya Uwekezaji ya NICOL imelazimika kufunga ofisi zake kutokana na migogoro inayoendelea miongoni mwa wana hisa huku ikihakikishia wanahisa usalama wa amana zao.

Hata hivyo wanahisa wa kampuni hiyo wamehakikishiwa kwamba amana zao ziko salama na thamani yake imeongezeka kutoka Sh bilioni 8.5 hadi Sh bilioni 65.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Bodi ya NICOL, Felix Mosha alisema wamelazimika kufunga ofisi zake ziliko kwenye jengo la Raha Tower miezi mitatu iliyopita, kutokana na akaunti za kampuni hizo kuzuiwa na Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA) zisifanye kazi kutokana na mgogoro uliosababisha kufunguliwa kwa kesi mahakama kuu.
Mosha alisema pamoja na matatizo wanayokabiliana nayo, amana za NICOL zimeongezeka kutokana na uwezekaji walioufanya kwenye Benki ya NMB, Kiwanda cha Nyama Dodoma  na uuzaji wa hisa zake kwenye kampuni ya Bayport. "Hivyo sio kweli kwamba Nicol iko kwenye hali mbaya ya kifedha, tuko vizuri," alisema.
Akifafanua, Mosha alisema Nicol  ni kampuni ya tatu kwa uwekezaji katika Benki ya NMB baada ya Exim Bank na TCCIA na amana zake zimekua kwa kasi. Pia alisema kiwanda cha nyama cha Dodoma   sasa mauzo ya kiwanda hicho ni Sh bilioni 2.1 na faida inayopatikana kila mwaka ni Sh milioni 800.
"Tumekigeuza kiwanda kilichokuwa kinapata hasara na sasa kinapata faida, haya ni mafanikio kwa NICOL," alisema Mosha na kuongeza kuwa walinunua hisa kwenye kampuni ya BayPort kwa Sh milioni 400 na wakauza hisa hizo kwa Sh milioni 500.
Alisema uwekezaji mwingine waliufanya kwenye kiwanda cha samaki cha Mwanza na uendeshaji wake ulikuwa mzuri; lakini wameamriwa na CMSA kusimamisha shughuli za kiwanda hicho hadi hapo mgogoro ndani ya NICOL utakapomalizika.
Mosha alikiri kuwa uwekezaji pekee ambao wamewekeza na kiwanda kinasuasua katika uendeshaji ni kwenye Kiwanda cha Dawa cha Moshi. Hata hivyo, hakutaka kueleza kwa undani hasara hiyo.
Mwenyekiti huyo wa bodi alisema kuanzia mwaka 2010 walitarajia waanze kutoa gawio, lakini mgogoro uliopo ndani ya NICOL umesababisha suala hilo lisifanyike kwa sasa hadi hapo kesi zilizoko mahakamani zitakapomalizika kusikilizwa.
Alisema bodi yake inachofanya kwa sasa ni kuweka hesabu vizuri na kesi itakapomalizika wataitisha mkutano mkuu wa wanahisa, ambao watatoa taarifa ya fedha na ndio watakaochagua bodi nyingine ya uendeshaji wa kampuni hiyo.

No comments: