BODI YA MIKOPO SASA KUKUSANYA MAREJESHO KUPITIA M-PESA...

Huduma ya M-Pesa.
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza kuanza kutumia huduma ya M-Pesa kukusanyia marejesho ya mikopo kutoka kwa wanufaika,  ili  kuimarisha makusanyo ya urejeshaji wa mikopo hiyo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi, Asangye Bangu, amewaambia waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo mpya jijini Dar es Salaam jana, kwamba Bodi inaendelea kujipanga kuhakikisha inaboresha njia za urejeshaji mikopo, ili kuwapatia walengwa urahisi.
Walengwa hao watatakiwa  kupiga *150*00# na baada ya hapo watapewa maelekezo na kufanya mrejesho yake wakati wowote mahali popote.
Alisema moja ya kazi za Bodi ni kusimamia utoaji wa mikopo kwa wanafunzi waliodahiliwa katika vyuo vya elimu ya juu, pamoja na urejeshwaji wa mikopo iliyotolewa na Serikali kwa waliokuwa wanafunzi wa elimu ya juu kuanzia 1994 mpaka sasa kwa nia ya kuufanya mfuko wa Elimu ya Juu kuwa endelevu.
"Tunayo furaha kubwa sana leo (jana) kutangaza kwamba   wanufaika wa mikopo ya Bodi wana uwezo wa kutumia mfumo wa M-Pesa kufanya marejesho ya mikopo yao moja kwa moja kwa Bodi," alisema Bangu.
Bingu alisema bodi ina imani kuwa M-Pesa itawapatia urahisi wanufaika, wa kutimiza wajibu wao kisheria wa kurudisha mikopo waliopatiwa kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu.
Wanufaika wa mikopo wanapaswa kuanza kurejesha mikopo yao mara baada ya miezi 12 kuanzia wanapohitimu masomo ya elimu ya juu au wanapositisha masomo kwa sababu yoyote ile, akiwa ameajiriwa ama hajaajiriwa.
Bingu alisema wanufaika walioajiriwa wanalipa mikopo yao kupitia kwa waajiri wao ambapo hukatwa marejesho ya mikopo kwenye mishahara yao ya kila mwezi, na mwajiri huwasilisha makato hayo kwenye Bodi kupitia   akaunti zake huku wale ambao sio waajiriwa, hutakiwa kuwasilisha marejesho ya mikopo katika benki za bodi.
Meneja Uhusiano wa Nje wa Vodacom, Salum Mwalim alisema kuzinduliwa kwa huduma hiyo ni mwendelezo wa namna huduma ya M-Pesa inavyorahisha miamala nchini kuzidi kuwa rahisi.
"M-Pesa imekuwa suluhisho la changamoto nyingi zinazohusu malipo ama miamala mingine ya kijamii na kibiashara," alisema Mwalim.

No comments: