BALOZI WA MAREKANI AMALIZA MUDA WAKE NCHINI, AAGA WATANZANIA...

Balozi Alfonso Lenhard.
Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhard amemaliza muda wake baada ya kutumikia kipindi cha miaka minne na kusema Tanzania iko moyoni mwake na ataendelea kuwa balozi wake popote atakapokuwa. 

Rais Jakaya Kikwete amesema katika kipindi hicho cha utumishi wa Lenhard, Tanzania na Marekani zimeimarisha uhusiano.
 "Asante kwa kazi nzuri ulioifanya katika kipindi chote cha miaka minne ulioitumikia hapa Tanzania. Mambo mengi na makubwa yenye kuleta maendeleo na manufaa kwa Tanzania yamefanyika hapa nchini na umeyasimamia na kuyafanikisha ipasavyo," alisema.
Kikwete alisema hayo jana wakati balozi huyo alipofika Ikulu kuaga na kumshukuru Rais na serikali  yake kwa ushirikiano alioupata katika kipindi chake cha ubalozi nchini.
Kwa upande wake, Balozi Lenhart alisema, "Nikushukuru wewe mheshimiwa Rais na serikali yako kwa ushirikiano mzuri na utayari wa kunisikiliza na kunisaidia wakati wote nilipohitaji ushauri wako,  umekuwa msaada mkubwa kwangu. Asante kwa ushirikiano wako na siku zote nitaendelea kuwa balozi wa Tanzania kwani Tanzania iko moyoni mwangu".
Mapema Balozi Lenhardt alipata nafasi ya kumtakia Rais Kikwete siku njema ya kuzaliwa na kumpatia zawadi kama kumbukumbu ya siku hiyo ya jana. Baada  ya mazungumzo, walipata  nafasi ya kula chakula cha mchana pamoja na mama Salma Kikwete na  mama Jacqueline Lenhardt, ambaye ni mke wa balozi Lenhardt.

No comments: