Katie Gee na Kirstie Trup. |
Raia wawili wa Uingereza waliomwagiwa tindikali Zanzibar, wameahidi kurudi visiwani humo afya zao zitakapoimarika.
Balozi wa Uingereza nchini, Diana Patricia Melrose alisema wasichana hao wanaendelea vizuri na kwamba wameahidi kurudi nchini.
Katie Gee na Kirstie Trup ambao ni walimu wa kujitolea, waliokuwa wakifundisha katika shule ya Kanisa la Anglikana iliyoko Mkunazini, Unguja, walimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana wakati walipokuwa katika matembezi jioni maeneo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Balozi Melrose alitoa taarifa hiyo mwishoni mwa wiki, alipozungumza na waandishi wa habari akielezea mikakati ya nchi za Afrika ya Mashariki kupambana na vitendo vya ugaidi.
"Wanaendelea vizuri na matibabu...wameahidi kurudi tena nchini mara wakati watakapokamilisha matibabu yao na kupona moja kwa moja," alisema.
Balozi huyo alisema nchi za Afrika, zinatakiwa kukabili matukio mbali mbali ya hujuma na ugaidi, ambayo athari zake ni kubwa kwa jamii na taifa.
Alitoa mfano wa tukio la ugaidi nchini Kenya la hivi karibuni, ambalo jengo la Westgate lilivamiwa, na kusema linatakiwa kuchukuliwa kwa hadhari kubwa na nchi nyingine za Afrika ya Mashariki katika mbinu na njia za kujilinda na matukio husika.
Wakati huo huo, alikabidhi vifaa mbali mbali vya ukaguzi na usalama vya kutambua mizigo na vifaa vingine na silaha pamoja na uingizaji wa dawa ya kulevya.
Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk alisema usalama katika viwanja vya ndege ni muhimu kwa ajili ya kudhibiti matukio mbali mbali ya uhalifu na ugaidi.
Alisema Zanzibar imejizatiti kuhakikisha kwamba viwanja vyake vya ndege, vinakuwa salama kwa ajili ya kuimarisha na kukuza sekta ya Utalii nchini.
"Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejizatiti kuhakikisha kwamba viwanja vyake vya ndege vinakuwa salama na matukio ya uhalifu, ikiwemo ugaidi kwa ajili ya kuimarisha sekta ya utalii," alisema.
Mbarouk aliipongeza Serikali ya Uingereza kwa msaada wake mkubwa, ambao umelenga kudhibiti uhalifu na usalama katika uwanja wa ndege wa Zanzibar.
Aliwataka wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume, kuvitumia kikamilifu kwa ajili ya kufichua vitendo vya uhalifu pamoja uingizaji wa dawa za kulevya.
No comments:
Post a Comment