Kanisa. |
Kumeibuka matapeli wanaotumia makanisa kuwaibia watu fedha kwa kuwadanganya kuwa fedha zao zitaombewa na kupata mara tatu zaidi ya kiwango walichonacho, pamoja na zawadi ya madini.
Aidha baadhi ya makanisa likiwemo Kanisa Katoliki na baadhi ya makanisa ya Pentekoste mkoani Pwani na jijini Dar es Salaam, yamejikuta yakitumiwa kwa utapeli huo na waliotapeliwa kuachwa wakilia nje ya milango ya makanisa hayo.
Mkoani Dar es Salaam, mwandishi amebaini kuwepo kwa utapeli huo ambapo baadhi ya watu katika maeneo ya Buguruni walitapeliwa kwa nyakati tofauti katika kipindi cha miaka miwili sasa kwa kuelezwa na matapeli hao wanaodaiwa kuwa na dawa za kuwapumbaza akili, wawape fedha ili wakaziombee.
"Zaidi ya watu 20 walitapeliwa Dar es Salaam mwaka jana, wanafuatiliwa na matapeli wakitoka ama benki, au kwenye mitandao ya simu kutoa fedha, wanaingizwa mjini kuwa fedha zao zitayeyuka ikiwa hawataziombea.
"Wanapelekwa mpaka kanisani na wanarubuniwa kwamba mchungaji ataziombea na mwenye fedha atapokea kutoka kwa Mungu, mara mbili ya fedha hizo baada ya siku kadhaa, kumbe ndio katapeliwa hivyo," alieleza polisi mmoja wa kituo cha Buguruni ambaye hakutaka jina kuandikwa jina lake kwa kuwa si msemaji.
Hivi karibuni, tukio kama hilo limebainika kuibuka kwa kasi mkoani Pwani, ambako watu takribani 10 wanaelezwa kutapeliwa fedha kati ya Sh 300,000 hadi milioni moja kila mmoja baada ya kutakiwa na matapeli kuwapatia fedha hizo ili wazipeleke kanisani kuombewa na baada ya siku moja, watapokea mara tatu na zawadi ya madini ya dhahabu (jiwe moja).
Inadaiwa makanisa kadhaa yamekumbwa na hili mkoani humo likiwemo Kanisa Katoliki ambapo katika Parokia ya Mtakatifu Don Bosco, Kibaha-Tumbi, zaidi ya watu wanne kati ya zaidi ya 10 wanaodaiwa kutapeliwa, walilizwa kupitia kanisa hilo.
Paroko Msaidizi wa Parokia hiyo, Padri Romwadi Mkandala akihubiri katika Misa ya kumuombea marehemu Sabina Nandi (92) katika Kijiji cha Boko-Timiza, Kibaha mkoani Pwani wiki moja iliyopita, alitoa tahadhari kwa waumini na wakazi wa Kibaha kuwa macho kutokana na kuibuka kwa utapeli huo.
"Tena kabla sijaendelea sana, jamani nyie watu mnaopenda fedha za bure bure, muwe macho, kuna matapeli wameibuka hapa Kibaha Tumbi, mtalizwa? Hivi kwa usawa huu nani akupe fedha za bure?
"Kuna watu wanadanganya fedha zinaombewa na mapadri kanisani kwetu, nasema hakuna kitu kama hicho, watu wamelizwa karibia 10, narudia tena hakuna kanisa wala msikiti utaombea pesa zako ziongezeke mara tatu kimiujiza, huo ni uvivu na wengi mtatapeliwa msipokuwa macho," alisema Padri Mkandala.
Akifafanua alisema hivi karibuni, watu wawili kila mmoja kwa wakati wake, walikutwa nje ya lango la kanisa hilo wakilia na kuhamaki baada ya kubaini kuwa wamelizwa kiasi kikubwa cha fedha na matapeli hao. Wengine walishawahi kukutwa lakini hawakuwa tayari kujieleza kutapeliwa.
Akielezea wanavyofanya, Padri Mkandala alisema kwa mujibu wa watu waliowahoji baada ya kuwakuta nje ya lango la kanisa wakilia, walieleza kuwa matapeli hao wanajipanga kuanzia katika vibanda vya kutolea fedha vya mitandao ya simu, ama katika benki na wakishajua kiasi cha fedha walichonacho huwafuatilia na kuanza kuwatapeli.
"Tuliowahoji pale kwetu walisema walienda benki, Tawi la NMB Kibaha siku ya tukio na baada ya kutoka benki, watu wawili waliwafuata na kuwaeleza kuwa Mungu amewaonesha kuwa wana hela nyingi na kama hawataziombea, zitapotea zote na watakuwa masikini milele, lakini wakiziombea, watapokea mara tatu ya kiwango walichonacho na kupewa zawadi ya madini kutoka mbinguni," alieleza Padri Mkandala katika ibada hiyo.
Mapema wiki hii akizungumza na gazeti hili, Padri Mkandala alifafanua kuwa matapeli hao huwarubuni kwa mazingaombwe watu hao mpaka wanakubali kuwapa fedha angalau robo tatu ya kiasi walichonacho na wanawaeleza wanazipeleka kanisani pamoja, kuwakabidhi mapadri wanaofanya kazi hiyo maalumu ya kuziombea usiku kucha na asubuhi wataenda kuzichukua zikiwa mara tatu ya kiwango cha awali.
Kwa mujibu wa Padri Mkandala anayefanya kazi na Paroko wa kanisa hilo, Padri Beno Kikudo, matapeli hao hutaja kwa uhakika majina yanayofanana na majina ya kweli ya mapadri hao na hufika na wahusika mpaka lango la kanisa na kuwataka wasubiri ili wao waingie ndani na fedha kuzikabidhi tayari kwa kuombewa.
"Matapeli huingia na fedha na baada ya muda mfupi hutoka, unajua mazingira ya kanisani mtu akiingia huwezi kuanza kumuhoji anakwenda wapi, maana ni mahali pa sala, wakitoka huwaendea wenye fedha na kuwaambia Padri kasema tuje kesho alfajiri zitakuwa zimeombewa na utapata mara tatu na zawadi ya madini, wanawaambia sisi tumetumwa na Mungu kuwasaidia kuondokana na umasikini," alieleza Padri Mkandala.
Alisema alfajiri inapofika, walinzi huwakuta watu hao getini au kwenye picha ya Bikira Maria, wakisubiri waliozipeleka kuombewa wafike. "Hukaa zaidi ya saa tatu na wakiwapigia simu hazipatikani na hapo huanza kuchanganyikiwa kwamba wameibiwa na kuanza kutaharuki na wengine kulia, tuliowahoji walisema walitajiwa majina ya Padri Raymond (badala ya Romwadi) na Padri Benckson (badala ya Beno).
Padri Mkandala alisema watu waliowakuta getini mwa kanisa, walidai kutapeliwa kati ya Sh 300,000 hadi milioni moja na baada ya kugundua wametapeliwa, kanisa liliwaelekeza kwenda kutoa taarifa Polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alipoulizwa kuhusu utapeli huo, alisema hakuna kesi iliyoripotiwa na kuelezea huenda wahusika wanaogopa kuripoti Polisi kutokana na mazingira ya kizembe ya kutapeliwa kwao.
"Tumejaribu kufuatilia matukio ya wiki chache zilizopita hapa kwetu, tumekosa kabisa matukio ya aina hiyo, huenda wahusika wanadai wameripoti kwetu lakini wanaogopa kuja maana ni uzembe gani huo wa kutapeliwa namna hiyo katika maisha ya leo, watu wanapenda fedha zisizo na jasho ndio madhara yake, kweli hawajaja kwetu bado, wakija nitawajulisha," alisema Kamanda Matei.
No comments:
Post a Comment