Abiria wa treni ya Reli ya Kati wakisubiria usafiri. |
Pamoja na nia njema ya Serikali ya kuhakikisha abiria wa treni ya Reli ya Kati wanakuwa na uhakika wa kusafiri angalau mara mbili kwa wiki, imedhihirika kuwa usafiri huo ni zaidi ya mateso kwa abiria wake.
Wengi wa abiria hao husafiri kati ya Dar es Salaam na mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Kigoma na hata Shinyanga na Mwanza.
Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na gazeti hili umebaini kuwa, abiria kwa sasa wamekuwa wanasafiri kwa mazoea na wengine kutokana na unafuu wa bei, lakini si kwa kufurahia usafiri wa treni kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na uchakavu wa injini za treni za abiria, ambazo hazina nguvu kiasi cha kuzifanya zisafiri kwa mwendo mdogo hivyo mara kadhaa kuwa nje ya ratiba ya safari.
Mathalani, safari ya Dar es Salaam ÐKigoma ambayo hupaswa kuchukua saa zisizozidi 36, sasa abiria wake hulazimika kusafiri hadi saa 54.
Pamoja na uchakavu wa injini hizo ambazo vyanzo vyetu vinakiri ni `bora liendeÕ kutokana na kutengenezwa zaidi ya miongo minne iliyopita, mabehewa ya abiria pia yamechakaa.
Hali ni mbaya zaidi kwa abiria wa daraja la tatu ambao ndio wengi zaidi. Katika madaraja yao, msongamano ni mkubwa mno, mathalani, behewa moja linalopaswa kuchukua abiria 80 walioketi kwenye viti chakavu, huchukua hadi abiria 200, huku wakiwa na mizigo iliyotapakaa kila sehemu. Wapo wanaodiriki kulala chini ya viti, hivyo kuwazuia waliokaa kupata fursa hata ya kukunja miguu.
Ni nadra kwa mtu kuvuka kutoka behewa moja kwenda jingine kutokana na msongamano, wengine wakikosa sehemu za kuweka mizigo na hivyo kuishia
kuibeba kichwani usiku na mchana.
Kwa wazoefu wa safari, pengine kwa kuijua adha hiyo, huwahi mapema maeneo ya karibu na vyoo na kuijaza mizigo yao huku wenyewe wakipiga kambi hapo.
Mwandishi alilazimika kufunga safari kutoka Dar es Salaam hadi Kigoma ili kushuhudia adha na raha za usafiri wa treni kwa Reli ya Kati, ulibaini kuwa hali ya msongamano ambayo si rafiki ni shubiri zaidi kutokana na joto kali ndani ya mabehewa ambayo feni zake za juu zimechakaa kiasi cha kutofanya kazi.
Aidha, kwa upande wa daraja la tatu, matumizi ya vyoo ni anasa kwani hakuna huduma ya maji, hali inayochangia kuwapo kwa uchafuzi mkubwa wa mazingira wakati wa usafiri.
Nafuu hupatikana katika vituo vikubwa, mfano Morogoro na Tabora ambayo kutokana na treni kusimama kwa kati ya saa moja na mawili, abiria hukimbilia kujisaidia au kuoga katika vyoo na mabafu ya kulipia katika maeneo hayo. Kwa ujumla, safari kati ya Dar es Salaam na Kigoma ina vituo vikubwa na vidogo jumla ya 85.
Haishangazi kuona abiria walioshuka kwenye treni wakiwa katika foleni za kulipia Sh 200 ili kuingia chooni, na wengine Sh 400 ili kupata nafasi ya kuoga. Kuna huduma ya sehemu ya kupiga mswaki, kunawa uso ambazo ni rahisi, kwani mtejwa hutozwa Sh 100.
Kwa abiria wa madaraja ya kwanza na pili, kwa kiasi fulani wana nafuu ya vyoo vyao kuwa na maji, ingawa vinaandamwa na hali ya uchafu. Huko nako, kuoga ni mara chache kwani hali ya uchafu bado ipo. Hawa kwa kuwa wana nafasi, wanaweza kupiga mswaki na kunawa uso bila ya kulazimika kupanga foleni treni inapokuwa imesimama.
Tishio la wizi pamoja na mateso ya msongamano, ukosefu wa huduma kama za vyoo na pia hali ya joto, mateso mengine kwa abiria yanatokana na tishio la wizi.
Wakati wote, abiria huwa macho kwa hofu ya kuibiwa kutokana na kushamiri kwa matukio ya aina hiyo.
Mmoja wa maofisa wa Kikosi cha Polisi Reli ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini, aliliambia gazeti hili kuwa ni vyema kuchukua tahadhari hasa unapokuwa daraja la tatu.
"Hali ni mbaya sana, usione ule msongamano, wengine wanafurahia kwa sababu wapo kazini. Wanaibiana sana, ndiyo maana hata nyakati za usiku abiria hawalali hovyo kila mmoja akimhofia mwenzake," alisema na kudai hali huwa mbaya nyakati za usiku kutokana na wezi wa vituo vya njiani kupanda juu ya mabehewa na kukwapua mali za abiria.
Anavitaja vituo vya kati ya Kidete na Morogoro, Saranda na Tabora na maeneo ya Uvinza hadi Kigoma kuwa ni tishio mno kwa staili hiyo ya wizi wa kupanda juu ya mabehewa nyakati za usiku.
"Usiku lazima ufunge madirisha, ukishangaa utaibiwa kila kitu, kuanzia simu, laptop (kompyuta ndogo) na hata mabegi kwa akinamama. Jamaa ni wepesi sana," anazidi kusimulia.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia mmoja wa wezi akinaswa baada kuingia ndani ya treni kwa lengo la kuiba akitokea juu ya behewa, lakini akajikuta akiangukia mikononi mwa polisi waliovaa kiraia.
Ilikuwa usiku wa saa 4:00 katika eneo la Nguruka, wilayani Uvinza, Kigoma. "Unamwona huyu, ni miongoni mwa vijana hatari sana wanaosumbua abiria nyakati za usiku. Wanatumia zaidi ushirikina ili wasinaswe, lakini safari hii amefika. Tunakwenda naye mpaka Kigoma mjini akaozee polisi," anasema ofisa mwingine.
Na kweli, mpaka treni inafikia mwisho wa reli Kigoma baada ya safari ya saa 54 kutoka Dar es Salaam, kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Ayoub, alikuwa mikononi mwa polisi.
Baadhi ya abiria waliozungumza na mwandishi wakiwa safarini walisema kuwa kwa abiria wa Kigoma hawana njia nyingine ya kukabiliana na hali hiyo kutokana na ukweli kwamba, ndio usafiri pekee nafuu na wa kuaminika kwenda ama kutoka mkoani humo.
Ingawa kuna usafiri wa mabasi machache yanayofanya safari kati ya Dar es Salaam na Kigoma, nauli zake ziko juu, kati ya Sh 65,000 na 75,000, wakati kwa abiria wa treni hulazimika kulipa Sh 27,700 kusafiri umbali wa kilomita zaidi ya 1,254 uliopo baina ya mikoa hiyo.
"Ni usafiri nafuu kwa walio wengi, ndiyo maana pamoja na hofu ya kutofika kwa wakati na adha nyingine za safarini, inasaidia. Hata hivyo nadhani Serikali inapaswa kutupia macho hali hii, ni mateso kwa kweli," alisema Gilbert Kaliza, mmoja wa wafanyabiashara anayetumia mara kwa mara usafiri huo kusafirisha bidhaa zake.
Pamoja na adha hizo, hali ya reli si nzuri, kwani nayo imechoka kiasi cha kuangusha mara kwa mara vichwa au injini za mabehewa ya mizigo, hali inayosababisha treni za abiria kucheleweshwa mara kwa mara ili kupisha behewa au kichwa cha treni kilichoanguka kiondolewe.
Mbali na adha hizo, pia inaponyesha mvua mabehewa yanavuja na watu kujikuta wakiloana ambapo mfano wa karibu ni juzi treni ilivyokuwa ikitoka Kigoma kuelekea Dar es Salaam ambapo watu walijikuta wakijikinga na mvua na wengine wakiloana.
Vilevile usafiri huo umekuwa na kero ya kujaa kunguni ambapo kwenye mabehewa ya daraja la pili ambayo yanatarajiwa kuwa na usafi yamejaa kunguni.
Masta Mkuu wa Shirika la Reli nchini (TRL) mkoani Kigoma, Ally Zunda hakuwa tayari kuzungumzia lolote juu ya matatizo husika, akisema wasemaji wapo makao makuu ya shirika jijini Dar es Salaam.
Alipotafutwa kwa njia ya simu, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe na Meneja Uhusiano wa TRL. Midladj Maez hawakupatikana.
Hata hivyo, Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa, inatafuta tiba ya kudumu juu ya uchakavu wa injini, mabehewa na njia ya reli ili kuufanya usafiri wa treni kuwa tegemeo la wengi zaidi mikoani inayotumia usafiri huo.
No comments:
Post a Comment