KASHFA!! SHULE YAENDESHWA MIAKA SABA BILA KUFANYIWA UKAGUZI...

Shule ya St Anne Marie ya Dar es Salaam inadaiwa kukaa takribani miaka saba bila kukaguliwa, hali ambayo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imeshutumiwa na kutakiwa kuimarisha kitengo chake cha ukaguzi kitekeleze majukumu yake.
Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza ambaye ni mmiliki wa shule hiyo, alisema hayo juzi na akashutumu pia kitendo cha  shule kulazimika kulipia gharama za wakaguzi.
"Mfano hapa shuleni,  hatujakaguliwa tangu mwaka 2005, wanakuja kukusanya fedha za ukaguzi bila kufanya ukaguzi, na si ndogo, tunalipa fedha nyingi kweli... wakija kudai fedha hizo tunatoa tu kwa shingo upande," alisema.
Alisema hayo juzi kwenye mahafali ya kidato cha nne ya shule hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo.
Bulembo aliungana na mbunge huyo kushutumu kitendo cha shule kutokaguliwa kwa kipindi kama hicho na kusema hiyo ni aibu na ni vigumu elimu bora kupatikana nchini bila kuimarisha kitengo cha ukaguzi.
Kwa mujibu wa Rweikiza, licha ya kuchangia mamilioni ya fedha kwa ajili ya ukaguzi, shule yake ya St Anne Marie ina miaka saba bila kukaguliwa ingawa kwa upande wa shule, wanao wakaguzi binafsi wawili ambao ni walimu waliobobea.
Aidha Rweikiza alilalamikia utitiri wa kodi kwa shule binafsi na kusema ni kero ambayo siyo tu inawagusa wamiliki, bali ina athari kwa wazazi na walezi wanaosomesha watoto shuleni hapo. “Hizi kodi zote zinalipwa na wazazi. Sisi hatuna fedha za kulipa,” alisema Rweikiza.
Wakati alisema zipo zaidi ya kodi 10 wanazopaswa kutoa, Rweikiza aliomba serikali kuangalia uwezekano wa kuzipunguza. Miongoni mwa kodi alizotaja na kushauri shule zipunguziwe mzigo, ni pamoja na kodi ya majengo ya mabango.
Rweikiza ambaye alisema zipo shule binafsi ambazo zimefungwa kutokana na gharama kubwa za uendeshaji, alisisitiza, "Gharama za uendeshaji wa shule binafsi ni kubwa mno, tunalipa kodi zaidi ya kumi, mbaya zaidi kodi hiyo inalipwa na mzazi...shule itatoa wapi?
Kuhusu  ufaulu wa wanafunzi,  mbunge huyo alilalamikia ushirikishwaji duni wa wadau katika uamuzi wa masuala muhimu katika mfumo wa elimu.
Alitoa mfano wa matokeo ya kidato cha nne mwaka jana, tatizo lilikuwa kwenye usahihishaji na upangaji matokeo ambao ulibadilishwa kimya kimya bila wadau kujulishwa.
Kwa mujibu wake, hivi karibuni wameletewa dodoso la elimu na wizara, ili wadau watoe maoni juu ya usahihishaji na viwango vya ufaulu na kushutumu kubwa limechelewa kuwafikia wakati wanafunzi wamekaribia kufanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne.
Bulembo aliahidi kufikisha malalamiko hayo serikalini yapate ufumbuzi. “Mimi mwenyewe nina shule zaidi ya 70 katika Jumuiya ninayoiongoza, kama hazikaguliwi tutapataje matokeo mazuri,” alisema.
Wakati huo huo, mwenyekiti huyo wa wazazi alikemea tabia ya wazazi na walezi kutoonesha mfano mwema katika malezi ya watoto wao.
Alitoa mfano wa mavazi na kusema baadhi ya wazazi na walezi wameshindwa kuwa mfano wa watoto wao. Alikemea kile alichosema tabia ya watoto kulelewa kama kuku wa kizungu ikiwa ni pamoja na kuvaa mavazi yasiyostahili.

No comments: