WATU WALIPUKIWA NA BOMU MAKABURINI WAKIADHIMISHA IDD EL FITR...

Mmoja wa watoto waliojeruhiwa kwenye mlipuko huo akipatiwa matibabu hospitalini.
Zaidi ya dazeni ya wanawake na watoto wameuawa makaburini nchini Afghanistan wakati wakitoa heshima zao za mwisho kwa ndugu zao waliofariki.

Bomu lililipuka jana kaburini katika wilaya ya kijijini kwenye jimbo la Nangarhar, lililoko mashariki mwa nchi hiyo.
Watu 14 waliuawa katika shambulio hilo, ambalo linaonekana lilipangwa kuingiliana na maadhimisho ya Idd El Fitr, kuhitimisha Mfungo wa Ramadhani.
Ni utamaduni wa watu wa Afghanistan kutembelea makaburi ya mababu zao wakati wa Idd kufanya mandari na kuwaenzi marehemu.
Waathirika wa bomu hilo la makaburini la Nangarhar wengi wao walikuwa kutoka kwenye familia moja, kwa mujibu wa msemaji wa gavana wa jimbo hilo.
Mbali na watu hao 14 waliokufa, mtoto mmoja na wanawake watatu walijeruhiwa katika tukio hilo.
Nangarhar na mji mkuu wake, Jalalabad, yamekumbwa na mfululizo wa milipuko ya mabomu na mashambulio ya kujitoa mhanga katika wiki iliyopita.
Kwingineko, walinzi watatu wa Mkuu wa Polisi wa jimbo la Helmand nchini Afghanistan, Mohammad Hakim Angaar, waliuawa Jumatano katika shambulio la bomu la kujitoa mhanga.

No comments: