MAPYA YAFICHUKA WALIMU WA UINGEREZA WALIOMWAGIWA TINDIKALI ZANZIBAR...

Walimu hao wakisaidiwa kuingia kwenye gari.
Wakati walimu wawili wa kujitolea, raia wa Uingereza, wakijeruhiwa kwa kumwagiwa tindikali, katika maeneo ya Mji Mkongwe, Shangani, Zanzibar, mapya yameibuka kuhusu walimu hao.

Kate Gee (18) na Kristie Trup (18),  walivamiwa na kujeruhiwa juzi saa moja usiku, wakienda kupata chakula cha jioni.
Habari za kuaminika zilizopatikana jana jioni zifichua kwamba mmoja wa walimu hao alishawahi kushambuliwa wakati akiwa kisiwani humo wiki mbili zilizopita.
Kwa mujibu wa mmoja wa marafiki zao, Oli Cohen, mwenye miaka 21, alisema: "Katie alishambuliwa wiki mbili zilizopita na mwanamke mmoja wa Kiislamu kwa kuimba wakati wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
"Alishitushwa mno na tukio hilo - lakini hakupatwa na hofu kiasi cha kufikiria kurejea nyumbani. Akaendelea kuishi hapo kumalizia safari yake na kazi yake ya kujitolea."
Akizungumza nje ya hekalu ambalo Kirstie anaishi na baba yake Marc na mama Rochelle, rafiki mwingine aliongeza: "Wamemaliza mchezo kwa sasa, inatia wasiwasi kiasi kuhusiana na kampuni ya bima na balozi mdogo.
Naibu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Yusuf Ilembo, alithibitisha jana wasichana hao kujeruhiwa kwa tindikali hiyo, na kusema ni sehemu  ya vitendo vya aina hiyo ya uhalifu vinavyoendelea Zanzibar.
"Tulipata taarifa ya tukio hilo jioni baada ya watu kumaliza kufuturu eneo la Shangani mjini hapa," alisema Kamanda Ilembo.
Taarifa zilizotufikia jana baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, zilieleza kuwa wasichana hao walikwenda Zanzibar kujitolea kufundisha kwa wiki tatu na juzi walikuwa katika wiki ya pili.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wakati walimu hao wakienda kupata chakula cha jioni, pikipiki aina ya Vespa, ilisimama mbele yao ikiwa na vijana wawili, mmoja wao aliwamwagia tindikali walimu hao.
Mwalimu Kate kwa mujibu wa taarifa hizo, alimwagiwa kifuani na mkononi huku Mwalimu Kristie akimwagiwa usoni na hali yake ilielezwa kuwa mbaya.
Kristie anatokea Hampstead na Kate ni mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Francis Holland mjini Chelsea.
Mama wa Kate, Nicky alisema familia hizo zinapambana kuwarejesha wanawake hao wawili nyumbani haraka iwezekanavyo.
Wachunguzi wanasema kundi la Waislamu ambao wanataka Zanzibar ijitenge kutoka Tanzania wanawezekana kuhusika na shambulio hilo lakini hakuna yeyote mpaka sasa aliyedai kuhusika na shambulio hilo.
Polisi imeanza uchunguzi wa tukio hilo, kwa nia ya kuwatia mikononi wahusika na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Matukio ya watu kumwagiwa tindikali ambayo sasa yanaonekana kuelekezwa kwa wageni, yanaweza kuathiri sekta ya utalii na sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)  imepanga kujitanua zaidi kupitia masoko ya Asia na Ulaya.
Wiki iliyopita, wakati Kamishna Mkuu wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ziwani,  alisema watuhumiwa wa shambulio la tindikali kama hilo dhidi ya Katibu wa Mufti, Shekhe Fadhil Soraga na Sheha wa Tomondo, Omar Mohamed Kidevu hadi sasa hawajakamatwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji kwenye Utalii Zanzibar (ZATI), Abdul Samad, aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP),  kwamba shambulio hilo linaweza kuathiri sekta hiyo Zanzibar.
Sekta ya utalii Zanzibar huchangia pato la Taifa kwa asilimia 50, huku ikichangia ajira kwa wananchi kwa asilimia 45.
Watalii kutoka Uingereza wanashika nafasi ya tatu kwa wingi Zanzibar kwa asilimia 20, wakiongozwa na Italia na Afrika Kusini.
Eneo la Mji Mkongwe linaongoza kwa kutembelewa na watalii wengi kujionea maeneo ya kihistoria na majengo ya kale kama Kanisa la Anglikana lililojengwa mwaka 1873 Mkunazini, ambalo ni kichocheo cha kuondoshwa kwa biashara ya utumwa mwaka 1907.
Rais Jakaya Kikwete alifika katika Hospitali ya Aga Khan jana mchana, ambapo alikwenda moja kwa moja katika chumba walimolazwa wasichana hao na kuzungumza nao na kupata taarifa ya maendeleo yao.
Baada ya hapo, alipita katika chumba alimolazwa Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo na kumjulia hali na kuzungumza naye.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya hospitali hiyo, Rais Kikwete alisema uvamizi huo ni wa kusikitisha na kushukuru uongozi wa hospitali hiyo kwa kuwahudumia vizuri wagonjwa hao.
Rais alisema ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama, kusaka wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Kiongozi wa Shirika la Art in Tanzania, lililoleta walimu hao nchini, Bashir Ismail, alisema inaonekana shambulio hilo lililenga walimu hao kutokana na aina ya mavazi waliyovaa.
Baada ya uvamizi huo, alisema waliwasiliana na Ubalozi wa Uingereza nchini, ambao ulipeleka ndege maalumu ikawasafirisha hadi Dar es Salaam ambako waliwasili hospitalini saa nne usiku.
Alisema katika eneo la tukio, kulikuwa na wageni wengi lakini waliomwagiwa tindikali hiyo ni walimu hao ambao walivaa suruali.
Kuhusu hali yao ya afya, Ismail alisema pamoja na majeraha, lakini wote wanazungumza na wakati wowote wakipata ndege, watasafirishwa kurejea kurudi nchini mwao Uingereza kwa matibabu zaidi.
Hivi karibuni mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa maduka ya Home Shopping Center (HSC), Said Mohamed Saad, alimwagiwa tindikali maeneo ya Msasani City Mall, Dar es Salaam na sasa yuko Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.
Alimwagiwa saa moja usiku, na mtu ambaye hakufahamika na mara baada ya tukio hilo, mhusika alikimbia huku mlinzi wa eneo hilo akijaribu kumkimbiza bila mafanikio baada ya kuteleza na kuanguka. Hatua hiyo ilitoa mwanya kwa mtuhumiwa kutoroka eneo la tukio kwa pikipiki.
Tukio hilo lilikuja takribani wiki mbili tangu Shekhe Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, Said Makamba kujeruhiwa  usoni kwa kumwagiwa tindikali usiku akiwa nyumbani kwake.

No comments: