Baadhi ya wanafunzi wa kike wakifua nguo zao. |
Baadhi ya wasichana wanaosoma katika Shule ya Sekondari Mzindakaya iliyopo kijiji cha Kaengesa, wilayani Sumbawanga, wametajwa kuishi kinyumba na wanaume ambao huwahudumia kwa kuwapatia mahitaji muhimu ikiwemo chakula, mavazi pia vileo.
Wanafunzi hao ni wale wanaoishi nje ya hosteli za shuleni hapo, wakidai wazazi wao hawana uwezo wa kulipa gharama za hosteli na hivyo kuamua kupanga vyumba maarufu kama 'magheto' nje ya maeneo ya shule.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi hivi karibuni kijijini hapo ilipo shule hiyo, ikiwa ni umbali wa zaidi ya kilomita 40 kutoka mjini Sumbawanga umebaini kuwa baadhi ya wanafunzi hao wa kike kutokana na kuwa huru kupita kiasi kwa kuishi katika 'magheto' wamejingiza katika 'ufuska' na ulevi wa pombe wa kupita kiasi.
"Si ajabu kukutana kijijini hapa siku za wikiendi na msichana wa shule akiwa amelewa pombe. Watoto hawa kwa kweli wameshaharibikiwa wengine ni walevi kupindukia," alisema mama mmoja kijijini hapo ambaye hakuwa tayari jina lake kuandikwa gazetini.
Pia uchunguzi wa mwandishi umebaini kuwa kuna mwingiliano mkubwa wa vijana wa kiume kijijini hapo wakitokea ndani na nje ya mkoa ambapo baadhi yao wanafanya vibarua katika kampuni ya ujenzi wa barabara ya Laela hadi Sumbawanga mjini ikipitia kijijini hapo yenye umbali wa kilomita 97 kwa kiwango cha lami.
Wengine wanadai kuwa ni walanguzi wa mazao ya nafaka hususani mahindi, lakini pia wapo vijana ambao ni maarufu kama wezi wa mafuta wanaodaiwa kuiba nishati hiyo ya kuendeshea mitambo na magari kutoka katika Kampuni hiyo ya ujenzi wa barabara hiyo kisha kuyauza kwa madereva wa magari makubwa na madogo kwa bei rahisi.
Inadaiwa kuwa kutokana na vijana hao wa kiume kuwa na uwezo fulani wa kifedha, huwapatia fedha vijana wa kiume wakazi wa kijijini hapo ili wawaunganishe na wasichana hao wanafunzi wanaoishi katika magheto.
Kwa mujibu wa baadhi ya vijana wa kiume walihojiwa na mwandishi wa habari hizi wamekiri kuwa kuwarubuni wasichana hao kuwahonga chakula, nguo pia kuwashawishi kunywa pombe ambapo baadhi yao wamejikuta wakiishi nao kinyumba kwa kuwapangishia nyumba kijijini hapa huku wakiendelea na masomo yao shuleni hapo kama kawaida .
"Hawa wanafunzi wa kike wanaishi katika 'magheto' wako huru sana hivyo kujikuta wakijiingiza katika tabia mbovu, zikiwemo za ukahaba, fikiri mwanafunzi wa kike kunywa pombe isitoshe hapa kijijini kuna nyumba za kulala wageni hakuna anayewazuia kulala humo na wanaume," alisema kijana moja wa kiume kwa masharti ya kutoandikwa jina lake.
Watoa taarifa hao kwa masharti ya kutoandikwa majina yao wamekiri kuwa wanaume wanaishi na wasichana hao kinyumba kwa siri, kwani huingia kwenye vyumba vya wasichana hao usiku kwa siri na alfajiri huondoka na kurejea wanakoishi ambapo wasichana nao hujiandaa kwenda shuleni.
Lakini pia uchunguzi wa mwandishi umebaini kuwa si wanafunzi wote wanaishi kwa kupanga vyumba kijijini humo wanatoka katika familia masikini, lakini pia wapo ambapo wazazi wao wanaojimudu kiuchumi na kuwachangia gharama za kuishi hosteli, lakini hukacha na kuishi kwa kupanga nyumba kijijini ili waweze kuwa huru zaidi .
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi hivi karibuni shuleni hapo, Makamu Mkuu wa shule hiyo, Agatha Okumu amekiri kuwa si salama kabisa kwa wasichana hao kuishi kwa kupanga vyumba kijijini hapo wakati mabweni yapo shuleni hapo kwa ajili yao.
"Kutokana na kuishi kwa kupanga vyumba kijijini hapa wanafunzi hao wa kike wamejikuta wakivamiwa na watu wasiojulikana usiku wakiwa wamelala na kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji ikiwemo kubakwa lakini hawasemi wanakaa kimya kisa eti wanaona aibu kusema kuwa wamebakwa.
Pia alikiri kuwa baadhi ya wazazi na walezi wanagoma kuchangia gharama za watoto wao kuishi hosteli shuleni hapo hivyo wanafunzi hao wanalazimika kupanga vyumba kijijini humo ambapo kodi ya chumba kwa mwezi ni Sh 1,000- hivyo kujikuta wakijiingiza katika tabia mbaya na baadhi yao wakishia kudhalilishwa kijinsia .
Naye Mkuu wa Shule hiyo, Nicholas Thomas alisikitishwa na wazazi wa watoto hao wa kike kukataa kuchangia gharama ili watoto hao waweze kuishi katika hosteli shuleni hapo, kwa madai kuwa wao ni masikini hawana uwezo wa kuchangia magunia mawili ya mahindi, debe moja la maharage na Sh 40,000 kwa mtoto mmoja aishi bweni kwa muhula mmoja .
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Shule, yapo mabweni mawili ambao yana uwezo wa kuchukua wanafunzi wa kike zaidi ya 200, lakini vyumba vingi viko wazi kwa kuwa wengi wao wamepanga vyumba kijijini.
"Shule hii ina wasichana 240 acha wavulana lakini wanaoishi hosteli ni 83 tena wameongezeka hivi karibuni baada ya wazazi wao kuvuna mazao shambani. Wazazi ni wagumu wanadai wao ni maskini hawawezi kumudu kuchangia gharama za watoto wao kuishi hosteli shuleni hapo tatizo hakuna sheria inayowabana," alisema.
Baadhi ya wanafunzi wa kike wa shule hiyo waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi wamekiri kuwepo kwa tabia hiyo waliyoiita 'chafu' miongoni mwao, lakini pia wanawalaumu wazazi wao kwa kushindwa kutimiza wajibu wao kama wazazi wao kwamba 'wamewatelekeza' kwa kukataa kuwagharimia ili waweze kuishi bwenini shuleni hapo kwenye usalama na malezi mazuri .
"Wazazi wetu si maskini kiasi hicho wametutelekeza sana na kutuacha kwenye" midomo ya simba tunakoishi kwenye magheto si salama kabia kwetu ... tunabakwa ovyo ovyo usiku , wengine 'tumeolewa' pia ni walevi sasa haya kweli ni maisha tunayostahili kuishi kama wanafunzi tena wa kike ?" alihoji mmoja wao "Mie nafikiria kuacha masomo bora nirudi nyumbani kuliko kuendelea kuishi kwa hofu ya kubakwa usiku haya si maisha haya kidogo," aliongeza.
Wasichana wa shule hiyo wanaoishi katika 'magheto' kijijini hapo wamejikuta wakikabiliwa na visa vya kuvamiwa na kubakwa mara kwa mara usiku ambapo hivi karibuni msichana mmoja alijiua kwa kunywa sumu ya panya baada ya kubakwa na mtu asiyejulikana pia wengine sita walinusurika kubakwa baada ya kuvamiwa usiku na watu wawili wasiofahamika ambao waliishia kuwacharaza marungu mwili kisha kuwaporoa kiasi cha Sh 2,100- taslimu na kutokomea kusikojulikana.
Habari za kipolisi kutoka Kituo Cha Polisi cha Mpui kilichopo kilomita 20 kutoka kijijini Kaengesa zinaeleza kuwa hakuna mtu yeyote hadi sasa aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo lakini msako mkali unafanyika kuwabaini watuhumiwa sheria iweze kuchukua mkondo wake.
2 comments:
Thanks for sharing your thoughts about ပုံစံ.
Regards
Everything is very open with a really clear clarification of the challenges.
It was truly informative. Your site is very helpful.
Thank you for sharing!
Post a Comment