WANAFUNZI 9,000 WAKATALIWA KUJIUNGA NA VYUO VYA ELIMU YA JUU...

Jengo la Nkrumah lililoko Chuo Kikuu cha Dar es Salaam eneo la Mlimani.
Wanafunzi 8,805 walioomba kujiunga na masomo ya shahada ya kwanza katika vyuo vya elimu ya juu nchini, kwa mwaka wa masomo 2013/2014, wamekataliwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Sifuni Mchome, alisema juzi katika taarifa ya tume hiyo kwamba wanafunzi hao hawakuchaguliwa kujiunga na vyuo vikuu kutokana na maombi yao kwa programu zote walizochagua, kukosa vigezo vilivyowekwa.
Alifafanua kukosekana kwa vigezo huko, kuwa ni pamoja na ushindani mkubwa wa wanafunzi katika baadhi ya programu walizochagua, ambao umesababisha wenye vigezo vya juu kupita na kujaza nafasi na wengine waliozitaka kukosa nafasi.
Sababu nyingine ya kukataliwa, imetajwa kuwa ni wanafunzi kushindwa kuwasilisha programu walizochagua na kuchagua programu ambazo hawana sifa nazo.
Hata hivyo, TCU imewapa nafasi nyingine wanafunzi hao, ili waombe tena lakini kwa kuchagua programu nyingine zisizo na ushindani, ambazo hazijajaa lakini pia ambazo wana sifa, kupitia mfumo wa udahili wa TCU na mwisho wa kuomba ni Agosti 9 mwaka huu. 
Wanafunzi hao wametakiwa kuangalia majina yao katika orodha ya wanafunzi ambao hawakuchaguliwa na TCU, inayopatikana kwenye tovuti ya taasisi hiyo ya www.tcu.go.tz na kufuata utaratibu uliowekwa kuomba upya.
“Baada ya mwanafunzi kuthibitisha jina lake kwenye orodha ya wanafunzi ambao hawakuchaguliwa iliyoko kwenye tovuti ya TCU, anatakiwa kuchagua programu moja tu kutoka kwenye orodha ya programu inayopatikana kwenye tovuti hiyo,” alisema Profesa Mchome katika taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa masharti hayo, pia mwanafunzi anatakiwa kufungua muongozo wa udahili unaopatikana kwenye tovuti hiyo, na kuthibitisha kwamba anayo sifa stahiki ya kujiunga na programu aliyoichagua.
“Baada ya kuwasilisha maombi yako, mfumo wenyewe utakutaarifu kuwa ama unastahili kuomba programu hiyo au la, na uchaguzi utazingatia kanuni ya wa kwanza ndiye atakayehudumiwa mwanzo.
“Programu moja itakapojaa, haitaoneshwa kwenye orodha ya programu zinazohitaji kujazwa kwenye mfumo wa udahili, hivyo mwombaji atatakiwa kujaza programu nyingine,” alisema Profesa Mchome katika taarifa hiyo.
Mwanafunzi atakayepata tatizo kuhusu maombi hayo, ametakiwa kuwasiliana na TCU kwa anuani au kupiga simu namba 0757 593868; 0757 594087; 0656 596822 na 0682 544832 au afike kwenye ofisi za tume zilizoko Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Wakati huo huo, muda wa kuomba mkopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu imefikia mwisho wiki iliyopita, Julai 30,  huku wanafunzi 17, 406 kati ya wanafunzi 115,431 walioomba mikopo hiyo, wakiwa hatarini kukosa.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Cosmas Mwaisobwa, amefafanua kwamba mpaka wakati wa kusitisha kupokea maombi kwa mwaka huu, wanafunzi 54,370 ambao ni waombaji mikopo wa mara ya kwanza walikwishakamilisha maombi yao.
Mbali na hao wa mara ya kwanza, Mwaisobwa aliyezungumza na mwandishi wiki iliyopita, alisema pia wanafunzi 61,061 wanaoendelea na masomo yao katika vyuo vya elimu ya juu, walituma maombi ya kutaka bodi hiyo kuendelea kuwakopesha.
Kutokana na hali hiyo, Bodi imejikuta ikipata maombi ya wanafunzi 115,431,  wakati ina bajeti ya kudhamini wanafunzi 98,025 kwa mwaka wa fedha 2013/14, ambayo hata hivyo ni ongezeko la asilimia 2.4.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, aliposoma bajeti ya wizara hiyo hivi karibuni, alisema Serikali kupitia HESLB, itatoa mikopo kwa wanafunzi 35,649 ambao ni waombaji wapya na 62,376 wanaoendelea.
Kwa bajeti hiyo, inaonekana wanafunzi wengi watakaokosa mikopo ni waombaji wapya, kwa kuwa wakati bajeti ya Serikali ilijielekeza kuwapa mikopo wanafunzi wanaoendelea 62,376, walioomba ni pungufu ya hao kwa kuwa wako 61,061.
Mwaka wa fedha uliopita, wanafunzi 98,773 waliwasilisha maombi na kati yao, 95,594 ndiyo waliopata mikopo.

No comments: