MAKADA WATANO WA CHADEMA WAFUTIWA MASHITAKA YA UGAIDI...

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, imefuta mashitaka ya ugaidi yaliyokuwa yakikabili makada watano wa Chadema na kubakiza mashitaka ya kummwagia tindikali kada wa CCM, Igunga, Musa Tesha.

Washitakiwa hao ni Evodius Justinian, (30) mkazi wa Bukoba, Oscar Kaijage wa Shinyanga, Seif Magesa wa Nyasaka, Mwanza, Rajabu Daniel wa Dodoma na Henry Kilewo wa Dar es Salaam.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Simon Lukelerwa alitoa hukumu hiyo jana na kusema upande wa mashitaka haukukidhi matakwa ya kisheria, wakati wakitetea hoja zao katika kesi ya ugaidi.
Baada ya kufuta mashitaka hayo, Jaji Lukelerwa aliamuru kesi hiyo ikiwa na mashitaka ya kummwagia tindikali kada huyo wa CCM, irudishwe katika Mahakama ya Wilaya ya Igunga.
Aliamuru  pia washitakiwa wote wapelekwe Igunga  kusikilizwa upya shauri lao, na kuongeza kuwa dhamana iko wazi kwa washitakiwa iwapo watakidhi matakwa ya Mahakama ya Wilaya  ya Igunga.
Kabla ya kusoma hukumu hiyo fupi, ulinzi uliimarishwa mahakamani ambapo askari Polisi wakiwa na silaha walionekana wakizunguka mahakamani hapo.
Kesi hiyo ya ugaidi ilifunguliwa Juni 24, baada ya washitakiwa hao kuachiwa awali Igunga, katika kesi ya kummwagia tindikali Tesha.
Julai 8 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Tabora, Hakimu Issa Magori, alisema hana mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kuiahirisha kwa muda.
Wakili wa upande wa utetezi katika kesi hiyo, Peter Kibatala, aliwambia waandishi wa habari, kwamba Mahakama Kuu imetenda haki na ana imani kubwa nayo.
Hata hivyo, alidai kwa kuwa washitakiwa hao walikamatwa katika sehemu tofauti, kesi zao zilipaswa kusikilizwa maeneo walikokamatwa.

No comments: