SHEKHE PONDA ARIDHIA KIFUNGO CHAKE CHA MWAKA MMOJA NJE...

Shekhe Issa Ponda akilakiwa na jamaa zake mara baada ya huku hiyo kwenye Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, jana.
Pamoja na kuhukumiwa kifungo, Katibu wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu, Shekhe Issa Ponda jana hakuonekana kusononeka na kusema kilichofikiwa na Mahakama ni haki yake.

Ponda alihukumiwa kifungo cha nje mwaka mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kuingia kwa nguvu kwenye kiwanja cha Chang'ombe Markazi kinachomilikiwa na Kampuni ya Agritanza.
Aidha, wafuasi wake 49 waliachiwa huru baada ya kuonekana hawana hatia kwa kuwa upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.
Washitakiwa hao walikuwa wanadaiwa kupanga njama, kuingia kwa nguvu kwenye kiwanja cha Chang'ombe Markazi, kujimilikisha kiwanja hicho, wizi wa mali zenye thamani ya Sh milioni 59 na uchochezi.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Victoria Nongwa alisema Shekhe Ponda alipatikana na hatia ya shauri moja kati ya matano yalikuwa yanamkabili na atatumikia kifungo cha mwaka mmoja nje, awe na tabia njema na asifanye kosa katika kipindi hicho.
Alisema kwa mujibu wa sheria, adhabu ya kosa la kuingia kwa nguvu ni kifungo kisichozidi miaka miwili pamoja na faini au faini peke yake, lakini alitoa adhabu hiyo kwa kuzingatia mshitakiwa kukaa rumande kwa muda mrefu, kutokana na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuzuia dhamana yake.
Katika mashitaka ya kuingia kwa nguvu katika kiwanja hicho, Hakimu Nongwa alisema ushahidi hauko wazi kama washitakiwa wengine walikuwa eneo hilo, isipokuwa Shekhe Ponda ambaye mashahidi wawili walithibitisha hilo na yeye kukiri.
Alisema katika utetezi, Shekhe Ponda alikiri kuingia eneo hilo kwa lengo la kujenga Msikiti wa muda, lakini hakuna ushahidi uliothibitisha kama aliingia kwa nguvu na anatiwa hatiani kwa kuwa kitendo cha kujenga Msikiti kilikuwa kinyume cha sheria.
"Shekhe Ponda na wenzake ambao hawafahamiki, waliamua kujenga Msikiti kwa lengo la kuzuia kiwanja hicho kuuzwa, baada ya kusikia Baraza la Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limebadilishana ardhi hiyo na eneo la ekari 40 lakini Shekhe Ponda alichukua hatua mkononi ," alisema.
Katika mashitaka ya kula njama yaliyokabili washitakiwa wote na la uchochezi lililowakabili Shekhe Ponda na Mukadam, Hakimu Nongwa alisema licha ya mashitaka hayo kutoeleza washitakiwa walipanga njama ya kutenda kosa gani, au kushawishi nini, upande wa mashitaka nao ulishindwa kuthibitisha na hakuna shahidi aliyeeleza hilo.
Aidha, alisema hakuna ushahidi wa kama washitakiwa waliiba na kutumia mali za ujenzi za Kampuni ya Agritanza kujenga Msikiti wa muda eneo hilo.
Alisema katika kesi hiyo upelelezi hakuwa mzuri kwa kuwa kuna mambo ambayo yaliibuka wakati wa utetezi na kuonesha washitakiwa walishiriki, hivyo upelelezi ungefanyika vizuri, washitakiwa wangepatikana na hatia.
Hata hivyo, alisema hawezi kuwatia hatiani kutokana na udhaifu wa utetezi kwa kuwa jukumu la kuthibitisha kesi ni la upande wa mashitaka.
Hata hivyo, alisema Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi za ardhi hivyo hatazungumza kama mabadilishano hayo yalikuwa halali au la, kwa kuwa Mahakama zinazoshughulikia ardhi ndizo zenye uwezo huo.
Hakimu Nongwa alisema hakuna ubishi kuwa kiwanja cha Markazi kilikuwa kinamilikiwa na Bakwata na baadaye kubadilishana, awali kilikuwa na ekari 20 na baadaye kiliuzwa bila kufuata utaratibu kikabaki ekari nne.
Bakwata ilibadilishana ardhi hiyo na eneo la ekari 40 la Kisarawe mkoani Pwani kwa lengo la kupata eneo kubwa la kujenga chuo na kutokana na hilo, Waislamu hawakuridhika na kufanya jitihada za kukirudisha.
Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani Oktoba 18 mwaka jana na kukana  mashitaka na kuachiwa kwa dhamana isipokuwa Shekhe Ponda na Mukadam ambao DPP aliwasilisha hati ya kuzuia dhamana yao.
Nje ya Mahakama baada ya hukumu, wafuasi wa Shekhe Ponda walibubujikwa na machozi huku wakirukaruka kwa furaha.
Aidha, baada ya Ponda kutoka nje ya Mahakama alipokewa kwa shangwe kubwa na wafuasi wake huku wakimzonga kila upande hali iliyosababisha askari Polisi kuingilia kati na kuamuru aingie katika gari lake na kuondoka eneo hilo.
Kabla ya kuondoka eneo la Mahakama, Ponda alisema hiyo ni haki yake kuwa nje na kwamba anaipokea kama haki yake  na si fadhila, ila inaonesha ni kwa kiwango gani vyombo vya Dola au vya usalama  vinatengeneza kesi nzito zisizo na ukweli wowote dhidi ya wananchi.
“Hali hii  ni  tatizo kubwa zaidi  hasa kunapokuwa na watendaji wa aina hii ambapo unasababisha kuharibu mfumo wa nchi kiusalama,” alisema Ponda na kuongeza kuwa vyombo vyenyewe uwezo wao wa maarifa ni mdogo, lakini  mashikinizo ya wanasiasa yanasababisha kutekeleza maelekezo hayo.
Alisema uamuzi wa kesi iliyokuwa ikimkabili  ni haki yake kuwa nje na    kuwa nje si fadhila na hakuna  mtu aliyemfadhili na anakwenda  kushiriki katika masuala mbalimbali na hivi karibuni atakuwa na fursa ya kuongea na wanajamii.
Baada ya kuzungumza maneno hayo Ponda aliongozwa na polisi na baadhi ya wafuasi wachache waliokuwa eneo hilo la Mahakama, kuingia katika gari lake aina ya Suzuki Trooper namba T306 BZF  na kuondoka chini ya ulinzi wa polisi akizuiwa kufika eneo la Maktaba ambalo lilikuwa na mkusanyiko mkubwa wa wafuasi wake.
Magari mawili ya Polisi yalimsindikiza kuelekea nyumbani ambapo mwenyewe alisikika akiwaambia polisi wapite barabara ya Bibi Titi Mohammed katika eneo walikokuwa wafuasi wake ili aweze kuwapungia mkono kama ishara ya kuwasalimia.
Wafuasi wake nao walisikika wakisema wanakwenda Msikiti wa Mtambani kumbusu na kumpongeza kiongozi wao huyo.
Msafara ulipofika Maktaba Kuu wafuasi walikusanyika, wakalipuka kwa shangwe huku wakikimbilia gari alilopanda Ponda na wengine wakitaka kulisukuma.
Hata hivyo, polisi waliwaamuru wakae mbali na msafara na kuondoka eneo hilo, tukio ambalo lilisababisha msongamano mkubwa wa magari huku wakazi wengi wa Dar es Salaam wakifuatilia tukio hilo wakiwa kwenye ghorofa.
Aidha, wakati kesi ikiendelea hata baada ya uamuzi kutolewa ulinzi ndani na nje ya Mahakama uliimarishwa.

No comments: