ATAKAYETAJA WALIORUSHA BOMU KANISANI ARUSHA KUZAWADIWA MILIONI 50/-...

IGP Said Mwema.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Inspekta Jenerali Saidi Mwema ameahidi kutoa donge nono  la Sh milioni 50 kwa atakayeweza kutoa taarifa ya kumfichua mhusika au wahusika wengine wa tukio la bomu lililotokea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi lililopo Olasiti jijini hapa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Liberatus Sabas, Mwema ameahidi kutoa zawadi hiyo ikiwa ni njia ya kushirikisha jamii kufanikisha jambo hilo kwa haraka zaidi pamoja na Polisi kuendelea na msako wake.
‘’Pamoja na jitihada zote zinazoendelea kufanywa na Jeshi hili, pia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini ameahidi kutoa zawadi ya Sh milioni 50 kwa yeyote atakayetoa taarifa ya kufichua mhusika/wahusika wengine wa tukio hilo,’’ ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Katika taarifa hiyo pia ilisema kuwa Polisi imekamata watu 12 wakiwamo raia wanne wa kiarabu kuhusika katika tukio hilo na wengine watatu kuwa ni siri kubwa kwa sasa.
Kamanda Sabas alitaja majina ya watu tisa tu waliokamatwa kuwa ni pamoja na Victor Kalisti (20) mwendesha bodaboda mkazi wa Kwa Mrombo, Joseph Lomayani (18) pia mwendesha bodaboda wa Kwa Mrombo.
Wengine ni George Silayo (23) mfanyabiashara wa Olasiti, Mohamed Sai (38) wa Ilala Dar es Salaam na Said Abdallah Said (28) raia wa Falme za Kiarabu Abudhabi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda Sabas wengine ni pamoja na Abdulaziz Mubarak (30) wa Saudia Arabia, Jassini Mbaraka (29) wa Bondeni Arusha, Foud Saleem Ahmed (28) raia wa Falme za Kiarabu na Said Mohsen wa Najran, Falme za Kiarabu.
Kamanda Sabas alisema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na jalada kuhusu tukio hilo limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwa uamuzi wa kisheria.
Alisema Polisi mkoani hapa imeimarisha ulinzi katika maeneo yote ya mkoa na hata leo siku ya maziko ya watu watatu waliolipuliwa na bomu, wananchi wasiwe na wasiwasi wajitokeze kwa wingi katika maziko hayo.
Mlipuko wa bomu ulitokea Mei 5 mwaka huu majira ya saa 4.30 asubuhi katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi lililo jijini Arusha eneo la Olasiti na kusababisha vifo vya watu watatu na 66 kujeruhiwa.
Siku ya tukio kulikuwa na uzinduzi wa Parokia mpya ya Olasiti katika kanisa hilo na mgeni rasmi alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini na pia ni Mjumbe wa Baba Mtakatifu Nchini, Askofu Mkuu Francisco Padilla.

No comments: