Dk Charles Kimei. |
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei amechaguliwa kwenye mchakato wa kumtafuta kinara wa Benki wa Afrika kwa mwaka 2013, unaoendeshwa na African Banker Awards chini ya African Development Bank Group.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana, kinara wa Benki wa mwaka ni tuzo inayotolewa kwa Viongozi (CEO`s) wa sekta ya benki na fedha barani Afrika, ambao wamepata mafanikio makubwa kwenye mashirika yao hivyo kuleta maendeleo katika sekta ya fedha na uchumi katika nchi zao na Afrika nzima kwa ujumla.
“African Banker Awards imechagua vinara watano wa sekta ya fedha katika Afrika nzima kuingia katika mchakato huo, ambapo mmoja wao ndiyo atakayejitwalia tuzo hiyo,” ilisema taarifa hiyo.
Zaidi ya Dk Kimei, wengine walioingia kwenye mchakato huo na nchi wanazotoka kwenye mabano ni Segun Agbaje wa GTB Bank (Nigeria), Aigboje Aig wa Imoukhede-Access Bank(Nigeria), Andrew Ally wa Africa Finance Corporation(Nigeria) na Jao Figuerdo wa Unico Bank.
Dk Kimei ni Mtanzania wa kwanza kuingizwa kwenye mchakato huu tangu kuanzishwa kwa tuzo hiyo zaidi ya miaka kumi iliyopita, na ni Mtanzania pekee kwenye kinyang`anyiro hicho, ambacho kimekuwa kikitawaliwa na benki kutoka nchi za Nigeria na Afrika ya Kusini.
Hii ni fahari kubwa kwa taifa letu kwani Dk Kimei ni Mtanzania anayeongoza benki kubwa ya Tanzania, inayoendeshwa na Watanzania wenyewe.
Kabla ya kujiunga na CRDB mwaka 1998 kama Mkurugenzi Mtendaji, Dk Kimei ambaye ni mchumi mwenye Shahada ya Uzamivu, amefanya kazi katika sekta ya fedha kwa zaidi ya miaka 30 akitokea Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alikokuwa Mkurugenzi wa Sera na Utafiti, Akiwa CRDB, ameiongoza benki hiyo iliyokuwa ikijiendesha kwa hasara hadi kuwa benki inayoongoza nchini.
Chini ya uongozi wake, CRDB imeweza kupata mafanikio makubwa, ikiwemo kutoka kutengeneza faida ya Sh bilioni mbili mwaka 1998 hadi kufikia Sh bilioni 108 mwaka huu. Pia, benki hiyo imeongeza mtandao wa matawi yake kutoka 16 hadi 97 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment