SARAFU MOJA AFRIKA MASHARIKI KATIKA HATUA ZA MWISHO...

Samuel Sitta.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta,  amewasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha huku akieleza mikakati iliyowekwa katika uanzishwaji wa Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaozifanya nchi wanachama kutumia  sarafu moja.

Waziri Sitta pia ameelezea hatua zilizofikia katika kuziwezesha nchi za Sudan ya Kusini na Somalia kuwa wanachama wa Jumuiya hiyo, akisema mpango huo upo katika hatua za mwisho.
Akisoma hotuba yake hiyo bungeni mjini hapa jana, Waziri Sitta alisema  katika kipindi cha mwaka 2012/ 2013, Wizara hiyo iliendelea kuratibu na kuongoza ushiriki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika majadiliano ya Itifaki ya Uanzishwaji wa Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Alisema majadiliano hayo yapo katika hatua za mwisho, ambapo pamoja na kupitia vipengele vyote vya rasimu ya Itifaki, nchi wanachama zimeandaa rasimu ya Mpangokazi wa kuelekea  katika Umoja wa Fedha.
“Kwa mujibu wa Mpangokazi huo, masuala ya msingi yatakamilika katika kipindi cha miaka 10 baada ya kukamilika kwa Itifaki.
“Mpango huo unalenga kuhakikisha kuwa misingi ya kuwezesha utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Fedha inakamilika kabla ya kuanza utekelezaji wa Itifaki hiyo,” alisema Waziri Sitta.
Alisema masuala ya msingi yaliyoainishwa katika Mpangokazi huo ni pamoja na kukamilisha hatua za awali za mtangamano za Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja na kuwianisha sera na sheria mbalimbali ili kufikia vigezo vya muunganiko wa uchumi mpana wa nchi wanachama na kuanzisha taasisi muhimu za kusimamia utekelezaji wa Umoja wa Fedha.
“Nchi wanachama zimekubaliana kuwa vigezo vya muunganiko wa uchumi mpana, vitumike kupima utayari wa nchi wanachama kujiunga na Umoja wa Fedha na kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wake.
“Vigezo vinavyopendekezwa ni kiwango cha juu cha mfumuko wa bei kisichozidi asilimia 8, kiwango cha juu cha nakisi ya bajeti ikijumuisha misaada kisichozidi asilimia 3 ya Pato la Taifa.
“Kigezo kingine ni kiwango cha juu cha deni la Taifa kisichozidi asilimia 50 ya Pato la Taifa na akiba ya fedha za kigeni ya kutosha  mahitaji ya miezi minne na nusu,” alisema Waziri Sitta.
Aidha alisema inatarajiwa kuwa majadiliano hayo yatakamilika Agosti mwaka huu na Itifaki itatiwa saini Novemba mwaka huu.
Somalia, Sudan Kusini kujiunga EAC Kuhusu maombi ya Jamhuri za Sudan Kusini na Somalia kujiunga na EAC, Waziri Sitta alikiambia Bunge kuwa katika mwaka wa fedha uliopita, nchi wanachama zilifanya uhakiki wa ombi la Jamhuri wa Sudan Kusini kujiunga na jumuiya kwa mujibu wa Ibara ya 3 (b) ya Mkataba wa Uanzishwaji wa EAC.
Alisema taarifa ya uhakiki iliwasilishwa katika Mkutano wa 14 wa wakuu wa nchi wanachama uliofanyika Novemba 2012 na kwamba baada ya kupitia, wakuu hao wa nchi waliliagiza Baraza la Mawaziri kuanza majadiliano na Sudan Kusini ili kuiwezesha kujiunga na jumuiya ambapo majadiliano yataendelea mwaka huu.
Kuhusu Somalia alisema nchi hiyo iliwasilisha maombi ya kujiunga na EAC mwaka 2011.
Alisema wakuu wa nchi katika mkutano wa 14 uliofanyika Novemba mwaka jana waliliagiza Baraza la Mawaziri la Jumuiya kufanya uhakiki wa endapo nchi hiyo inakidhi vigezo na kwamba kazi hiyo itafanyika mwaka huu.
Waziri Sitta aliomba Bunge kukubali kuidhinisha Sh bilioni 20.47 ili kuiwezesha Wizara hiyo ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutekeleza majukumu na malengo yake kwa mwaka ujao wa fedha ambapo kati yake Sh bilioni 19 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na Sh bilioni 1.47 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi. Bunge limepitisha bajeti hiyo.

No comments: