Sheha Mohammed Omar Said `Kidevu’. |
Matukio ya kujichukulia sheria mkononi yameendelea kujitokeza hapa, na juzi jioni Sheha wa Shehia (Kata) ya Tomondo Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja Mohammed Omar Said `Kidevu’ alivamiwa na watu wasiojulikana na kisha kummwagia tindikali ambayo imemjeruhi vibaya sehemu ya kifua na jicho la kulia.
Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mkadam Khamis Mkadam amethibitisha tukio hilo na kusema Sheha Omar ameumia vibaya sehemu ya kifua na jicho.
Akifafanua zaidi, alisema kwa sasa Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo. Inadaiwa aliyefanya kitendo hicho alificha sura yake kwa kuvaa soksi.
Mkadam alisema kwa sasa polisi wanashikilia chupa moja ikiwa na maji maji yanayosadikiwa kuwa ni tindikali iliyotumika kumjeruhi sheha huyo.
“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hili ambapo katika hatua za awali tunafanya uchunguzi wa chupa yenye maji maji yanayosadikiwa kuwa na tindikali,” alisema.
Kidevu (61) alipata kuwa mchezaji maarufu wa timu ya Taifa ya Zanzibar pamoja na timu ya Kikosi cha KMKM iliyotamba katika miaka ya 1976, kwa mujibu wa taarifa za aliyekuwa Katibu wa KMKM Mussa Soraga.
Daktari mmoja anayefanya kazi katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais ambaye alishiriki katika hatua za awali za kutoa matibabu, alisema sheha huyo ameumia sehemu ya jicho la kulia.
“Tumemfanyia matibabu ya kwanza na tumebaini kwamba ameumia vibaya sehemu ya kifua pamoja na jicho moja la kulia,” alisema.
Daktari Mwandamizi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Juma aliitaka Serikali kudhibiti matumizi ya tindikali dhidi ya mashambulizi ya binadamu.
“Serikali inatakiwa kuweka sheria kali kudhibiti matumizi ya tindikali kwa sababu yanaweza kuleta madhara makubwa ikiwemo watu kupata ulemavu wa maisha'' alisema.
Ofisa ambaye hata hivyo alisema si msemaji, kutoka Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anayeshughulikia tawala za mikoa, alithibitisha kupokea taarifa ya kujeruhiwa kwa sheha huyo wa Tomondo.
“Tumepokea taarifa ya kujeruhiwa sheha wa Tomondo na kwa sasa tunalifanyia kazi shauri hilo zaidi suala zima la matibabu yake,” alisema ofisa huyo.
Matukio ya watu kumwagiwa tindikali yanaonekana kukithiri Zanzibar. Mwaka jana, Naibu wa Mufti Mkuu Sheikh Fadhil Soraga alijeruhiwa vibaya kwa tindikali wakati akifanya mazoezi ya asubuhi hapo Mwanakwerekwe.
Aidha aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa, Rashid Ali Juma ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) naye alimwagiwa tindikali usoni na kifuani na kulazimika kusafirishwa hadi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam na baadaye kulazwa Aga Khan na kusafirishwa India kwa uchunguzi zaidi.
No comments:
Post a Comment