Kamanda Faustine Shilogile. |
Askari Polisi watatu kati yao wawili wenye cheo cha Sajini na mwingine Koplo wa Jeshi la Polisi mkoani Morogoro, wamefukuzwa kazi baada ya kufikishwa mahakama ya Kijeshi wakituhumiwa kushirikiana na raia kumbambikia mfanyabiashara fuvu la kichwa cha binadamu.
Wakati hayo yakijiri mkoani Morogoro, kwa upande wa Arusha, polisi aliyekufuzwa kazi hivi karibuni kwa tuhuma za kukutwa akisafirisha bangi magunia 18, ametoroka mikononi mwa polisi wakati akipekuliwa nyumbani kwake, nje kidogo ya Jiji la Arusha kabla ya kufikishwa mahakama ya kiraia.
Kwa upande wa askari wanaodaiwa kutumia fuvu kubambikia kesi, wamefikishwa katika mahakama ya kiraia, wakidaiwa kumbambikia mfanyabiashara Samson Mwita kwa kutumia fuvu wakitaka wapewe fedha suala hilo lisifikishwe polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, aliwataja askari hao ni D 4807 Sajini Sadick, D 4344 Sajini Mohammed wote kutoka Kituo cha Polisi Dakawa, wilayani Mvomero na E 3861 Koplo Nula wa Kituo cha Polisi Dumila, wilayani Kilosa.
Askari hao walifikishwa mahakamani wakiwa na mshirika wao Rashid Ally au Sharifu Hassan (47) mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam na kesi yao imepangwa kutajwa Juni 3, mwaka huu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa akisimulia tukio hilo lilitokea Mei 7, mwaka huu saa 12 :30 asubuhi katika mtaa wa Mgudeni, Kata ya Dumila, wilayani Kilosa, alisema askari hao watatu na raia huyo walikula njama ya utapeli kwa kumbambikizia mfanyabiashara maarufu kwa jina la ‘Mula’, fuvu linalosadikiwa kuwa la kichwa cha binadamu.
Hata hivyo alisema, askari hao walijipangia wenyewe kazi bila ya idhini ya wakuu wao na kwa kushirikiana na raia huyo waliamua kufanya vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya kazi ya kutaka kujipatia fedha kwa njia ya kubambikiza kosa mtu mwingine.
Hata hivyo alisema, uchunguzi bado unaendelea ili kubaini mtandao wa matapeli wanaoshirikiana na askari wa jeshi hilo na akawaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Polisi kwa kutoa taarifa na kuwafichua wahalifu na askari wanaokwenda kinyume na utendaji wao wa kazi.
Hata hivyo, ilidaiwa kuwa askari hao walimwambia mfanyabiashara huyo awapatie Sh milioni 25 kumaliza suala hilo kitu ambacho Mwita alikipinga na kuwataka kulifikisha suala hilo Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro.
Akizungumzia kutoroka kwa Koplo Edward aliyekamatwa mkoani Kilimanjaro akisafirisha bangi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema baada ya kufikishwa mahakama ya kijeshi ilikuwa afikishwe katika mahakama ya kiraia kujibu mashitaka hayo.
Kamanda alisema alitoroka wakati akipekuliwa nyumbani kwake na Ofisa wa polisi aliyekuwa akisimamia upekuzi huo, Inspekta Isack Manoni anahojiwa kuhusiana na kadhia hiyo.
Edward akiwa na mwenzake mwenye namba G.2434 Pc George walikamatwa Mei 18 mwaka huu saa 5 maeneo ya Himo wakiwa na magunia 18 ndani ya gari la Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) la Mkoa wa Arusha lenye namba za usajili PT 2025 Toyota Land Cruiser wakitoka Arusha kwenda Holili mpakani mwa Kenya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema askari hao walishafukuzwa kazi na hatua za kuwafikisha katika mahakama za kiraia zilikuwa zikiendelea kwa kosa la kufanya biashara haramu ya bangi.
Sabas alisema askari hao walipelekwa nyumbani kwao eneo la Mrombo nje kidogo ya jiji la Arusha, kwa ajili ya upekuzi ndipo Edward alitoroka na kuwakimbia polisi ambao hawakufanikiwa kumkamata.
No comments:
Post a Comment